Varane kuondoka Man Utd mwishoni mwa msimu

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alijiunga na kikosi cha Old Trafford kutoka Real Madrid msimu wa joto 2021

Muhtasari
  • "Kila mtu United anamshukuru Rapha kwa huduma yake na anamtakia heri kwa siku zijazo,"ilisema taarifa ya United.

Beki wa Manchester United Raphael Varane ataondoka katika klabu hiyo mkataba wake utakapokamilika mwishoni mwa msimu huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alijiunga na kikosi cha Old Trafford kutoka Real Madrid msimu wa joto 2021 kwa ada ya awali ya takriban £34m na amecheza mechi 93.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa aliisaidia United kushinda Kombe la Carabao mwaka wa 2023 wakati kikosi cha meneja Erik ten Hag kilipoifunga Newcastle United kwenye fainali.

"Kila mtu United anamshukuru Rapha kwa huduma yake na anamtakia heri kwa siku zijazo,"ilisema taarifa ya United.

KWINGINE NI KUWA;

14 wafariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya bango kuanguka India

Takriban watu 14 wameaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya bango kubwa kuanguka wakati wa dhoruba ya ghafla katika mji wa Mumbai nchini India.

Bango hilo, lenye ukubwa wa mita 70 kwa 50 kwa mujibu wa polisi, lilianguka kwenye nyumba na kituo cha petroli jijini siku ya Jumatatu.

Huduma za dharura zinasema watu wachache bado wamenaswa chini yake na shughuli ya uokoaji inaendelea.

Serikali ya jimbo la Maharashtra, ambako Mumbai iko, imeagiza uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.

Picha kwenye chaneli za habari za nchini zinaonyesha bango kubwa likiyumba kwenye upepo kabla ya kuacha njia na kuanguka kwenye majengo karibu na barabara yenye shughuli nyingi katika kitongoji cha mashariki cha jiji cha Ghatkopar. Magari kadhaa yalipondwa katika ajali hiyo.

Katika picha kutoka eneo la tukio, timu za dharura zinaweza kuonekana zikiondoa mabaki. Kanda za video zinaonyesha wafanyakazi wa uokoaji wakimtoa mwathiriwa kutoka chini ya ubao ulioanguka na kutumia zana za nguvu kukata chuma.

"Tumeokoa karibu watu 80 salama," afisa mmoja aliambia shirika la habari la ANI. "Kuna gari moja jekundu ambalo limeharibika vibaya, tunashuku kuna baadhi ya watu wamekwama ndani."