Ababu Namwamba:Hongera Gor Mahia kwa kunyakua taji la la ligi kuu ya Kenya 2023/24

Waziri wa michezo na masuala ya vijana amewapongeza mabingwa hao baada ya kushinda taji la ligi kuu ya Kenya siku ya Jumapili kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Muhoroni Youth

Muhtasari

• Gor Mahia ilishinda taji la ligi kuu ya Kenya kwa mara ya 21.

• Kogalo kwa sasa wamefuzu kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

WAZIRI WA MICHEZO ABABU NAMWAMBA
Image: TWITTER

Waziri wa michezo na masuala ya vijana Ababu Namwamba ametoa pongezi zake za dhati kwa Gor Mahia kwa mafanikio yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya 2023/2024.

Ushindi huo uliashiria taji la 21 la Kogalo la ligi na kujihakikishia nafasi ya kucheza msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ushindi  wa Gor Mahia  wa mabao 3-0 dhidi ya Muhoroni Youth kwenye uwanja wa SportPesa Arena mjini Murang'a,uliwakikishia taji hilo la 21 na kuwafanya wawe kileleni mwa ligi hiyo kwa pointi 67.Akitafakari ufanisi wa Gor Mahia,waziri Namwamba alisifu uchezaji thabiti wa timu hiyo.

"Hongera Kogalo kwa kunyakua taji la Ligi Kuu ya Kenya 2023/24. Taji lenu  la 21 la KPL linaimarisha nafasi yenu kama Wafalme wa Kenya ambao hawajapingwa," Namwamba alieleza kwenye ukurasa wake wa X almaarufu twitaa.

Waziri huyo pia alikubali mapambano ya awali ya timu hiyo na vikwazo vya FIFA, ambavyo hapo awali vilizuia ushiriki wao katika mashindano ya kimataifa, na alielezea matarajio yake ya siku zijazo.

"Tujiandae kwa wakati. Gor Mahia wameonja ushindi wa bara hapo awali, na ninaamini wanaweza kutwaa tena Afrika," aliongeza.

Msimu uliopita, wizara ya michezo na masuala ya vijana iliingilia kati kusaidia sio tu Gor Mahia bali timu nyingine katika ligi mbalimbali chini ya mpango wa tuzo za Hongera.

Gor Mahia ilipata usaidizi mkubwa wa kifedha, ikiwa ni pamoja na Ksh 10 milioni kutatua vikwazo vya FIFA, na kuwawezesha kurejesha hadhi yao katika soka ya bara. Timu zingine, zikiwemo Kakamega Homeboyz na Ulinzi Starlets, pia zilinufaika na mpango huu. Waziri huyo pia aliangazia juhudi zinazoendelea za serikali kubadilisha Ligi Kuu ya Kenya kuwa chombo cha kibiashara.

Aidha, Eliud Owalo, katibu wa baraza la mawaziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali, aliyehudhuria mechi hiyo, aliunga mkono maoni ya Namwamba. Owalo alisifu ubora thabiti wa Gor Mahia katika ligi na kueleza kujitolea kwake kuunga mkono maandalizi ya timu hiyo kwa ligi ya mabingwa Afrika ijayo.

"Kushinda ligi imekuwa jambo la kawaida kwa Gor Mahia; ni wakati wa kulenga zaidi na kutwaa taji la bara,"alisema Owalo