Kai Havertz aandika ujumbe wa kihisia baada ya Arsenal kushindwa kutwaa ubingwa wa EPL

"Itachukua muda kukabiliana na kila kitu lakini najua tukiwa na klabu hii tunaweza kufikia mambo makubwa." alisema.

Muhtasari

• Havertz alizungumzia jinsi klabu yake mpya imemsaidia kukuza taaluma yake ya soka katika mwaka mmoja uliopita.

•Katika msimu wake wa kwanza na Wanabunduki, amefunga jumla ya mabao 13 na kusaidia katika mabao 7.

Image: INSTAGRAM// KAI HAVERTZ

Kiungo wa kati wa Arsenal Kai Havertz aliandika chapisho la kihisia siku ya Jumatatu kufuatia kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza wa 2023/24 siku ya Jumapili.

Msimu wa EPL 2023/24 ulimalizika jioni ya Mei 19, wakati Mabingwa watetezi Mancehester City walipotwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo. Vijana wa Pep Guardiola walishinda klabu ya West Ham United 3-1 kwenye Uwanja wa Etihad na kujihakikishia kombe la mwaka huu wakiwa na pointi 91, huku Arsenal wakimaliza nafasi ya pili wakiwa na pointi 89 baada ya kuifunga Everton 2-1 kwenye uwanja wa Emirates.

Katika chapisho lake la siku a Jumatatu, Havertz alizungumzia jinsi klabu yake mpya imemsaidia kukuza taaluma yake ya soka katika mwaka mmoja uliopita.

Pia alitoa shukurani zake kwa mashabiki wa Arsenal, wakufunzi na wachezaji wenzake kwa sapoti waliyomuonyesha katika msimu uliomalizika.

“Nitaanzia wapi.. Msimu wangu wa kwanza umekuwa ambao umenisaidia kukua kama mtu na mchezaji kwa njia nyingi. Nashukuru sana kwa sapoti yote msimu huu, kutoka kwa mashabiki, wafanyakazi na wachezaji wenzangu wa timu,” Havertz alisema.

Aliongeza, "Itachukua muda kukabiliana na kila kitu lakini najua tukiwa na klabu hii tunaweza kufikia mambo makubwa."

Mshambuliaji huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 25 alijiunga na Arsenal kutoka kwa wapinzani wao wa London Chelsea mnamo Juni mwaka jana na amekuwa muhimu sana katika timu ya Mikel Arteta msimu huu. Hapo awali alitumika kama winga na kiungo wa kati lakini kuelekea mwisho wa msimu, Arteta amemtumia kama mshambuliaji.

Katika msimu wake wa kwanza akiwa na Wanabunduki, amefunga jumla ya mabao 13 na kusaidia katika mabao 7.