Firat afichua 'tikitaka' za kutumia kabla ya mechi dhidi ya Burundi na Ivory Coast

Mkufunzi huyo ameonyesha ujasiri jinsi ya kukabiliana na Burundi na Ivory coast kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia huku akielezea wachezaji ambao wamekumbwa na majeraha kabla ya mechi hizo

Muhtasari

• Harambee Stars wameanza mazoezi ya kujitayarisha kwa mechi za kufuzu kwa kombe l dunia 2026 

•Kenya itaendelesha kampeni dhidi ya Burundi  Ijumaa 7,Juni,2024

Kocha Mkuu wa Harambee Stars Engin Firat.
Kocha Mkuu wa Harambee Stars Engin Firat.
Image: Maktaba

Kocha wa Harambee Stars Engin Firat amedokeza kwamba huenda akalazimika kutumia wachezaji tofauti katika kila mechi mbili zijazo za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 mwezi Juni.

Harambee Stars watakuwa wenyeji wa Burundi na Ivory Coast nchini Malawi mnamo Juni 7 na 11 mtawalia katika Uwanja wa Kitaifa wa Bingu mjini Lilongwe.Firat anakiri kuwa mechi zote mbili zina changamoto tofauti ambazo zitahitaji mikakati mbalimbali. Firat anasema mabingwa wa Afrika Ivory Coast wana ubora zaidi na wataijaribu timu yake hadi hivyo hitaji la kusalia imara huku Burundi ikicheza mchezo wa kujilinda zaidi ambao utahitaji wachezaji wanaoweza penyeza kwa undani.

"Nahitaji kujua ni jinsi gani naweza kutumia nguvu za wachezaji wangu dhidi ya udhaifu wao mdogo na jinsi ya kuwasimamisha," Firat alisema wakati wa mkutano na vyombo vya habari Jumatano.

'Mipango miwili tofauti kabisa kwangu kwa hivyo lazima tutafute njia ya kujiandaa na tutajaribu kadri ya uwezo wetu kuwa tayari kwa zote mbili na inaonekana kama mechi zote mbili tutakuwa na wachezaji tofauti uwanjani."

Mkufunzi huyo pia ameelezea kukumbwa na majeraha miongoni mwa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza.Wachezaji hao ni pamoja na;mshambulizi Masoud Juma,mabeki Denis Nganga, Eric 'marcelo' Ouma na Joseph Okumu

"Sijui kwa hakika nani atakuwa tayari kwa asilimia 100." Firat alisema

 Aidha,Harambee Stars walikuwa wakitegemea uungwaji mkono wa nyumbani kuwasaidia kupata pointi nyingi zaidi kutoka kwa mechi zote mbili lakini italazimika kufanya hivyo bila wingi wa mashabiki.Kenya haina uwanja bora ulioidhinishwa na CAF na FIFA.

Kenya iko katika nafasi ya tatu katika Kundi F ikiwa na pointi tatu katika mechi mbili sawa na Burundi, huku Ivory Coast wakiwa kileleni kwa pointi sita, sawa na Gabon, huku Gambia, ambayo sasa itanolewa na kocha wa zamani wa Gor Mahia, Jonathan McKinstry, na Ushelisheli bado hawajarekodi pointi.