West Ham wamteua aliyekuwa kocha wa Real Madrid baada ya kuondoka kwa David Moyes

Klabu ya West Ham United imetangaza kumsajili kocha Julen Lopetegui.

Muhtasari

•West Ham imetangaza kuwa meneja huyo mwenye umri wa miaka 57 ataanza kazi yake ya ukocha Julai 2024.

•Aliwahi kuhudumu kama kocha katika klabu za Rayo Vallecano, Castilla, Porto, Real Madrid, Sevilla na Wolverhampton Wanderers.

imemteua Julen Lopetegui kuwa kocha mpya
Klabu ya West Ham imemteua Julen Lopetegui kuwa kocha mpya
Image: WESTHAM

Klabu ya West Ham United imetangaza kumsajili kocha Julen Lopetegui.

Julen alitangazwa kuwa kocha mpya wa Hammers siku ya Alhamisi, akichukua nafasi ya David Moyes ambaye aliondoka katika klabu hiyo Mei 19 baada ya kumalizika kwa EPL 2023/24.

"Tuma salamu kwa Kocha Mkuu mpya wa West Ham United. Karibu London, Julen Lopetegui!” West Ham ilitangaza kupitia akaunti rasmi za mitandao ya kijamii.

Julen anajiunga na klabu hiyo yenye maskani yake London miezi kadhaa baada ya kuondoka Wolverhampton Wanderers mwezi Agosti mwaka jana.

West Ham imetangaza kuwa meneja huyo mwenye umri wa miaka 57 ataanza kazi yake ya ukocha Julai 2024.

"Ninajisikia furaha sana, kwanza kabisa, kwa dhamira kubwa ya kuwa sehemu ya mustakabali wa klabu hii kubwa na kujaribu kuweka muhuri wetu kwenye jiwe na kuweza kufikia malengo yetu yote. Na kuwa bora na bora kila wakati kwa sababu mpira wa miguu unahusu hili," Julen alisema baada ya kujiunga na klabu.

Kabla ya kujiunga na West Ham, Mhispania huyo aliwahi kuhudumu kama kocha katika klabu za Rayo Vallecano, Castilla, Porto, Real Madrid, Sevilla na Wolverhampton Wanderers.

Mapema mwezi huu, West Ham ilithibitisha kwamba Moyes, ambaye alichukua mikoba yake ya pili katika klabu hiyo Desemba 2019 na kushinda Ligi ya Europa Conference mwaka 2023, angeondoka mwishoni mwa msimu.

Raia huyo wa Uskoti mwenye umri wa miaka 61 alikuwa chini ya shinikizo kubwa baada ya matokeo mabaya ambayo yaliwafanya The Hammers kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye Ligi ya Premia na kukosa msimu wa nne mfululizo barani Ulaya.