Erik ten Hag azungumza kuhusu kuondoka Man United baada ya fainali za FA

Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu meneja huyo huku baadhi ya ripoti zikidai ataondoka baada ya fainali ya FA.

Muhtasari

•Ten Hag alidokeza kwamba sasa anaangazia mchuano wa Jumamosi na sio kile kinachotokea baada ya hapo.

•Pia alizungumza kuhusu miradi inayoendelea katika klabu hiyo akidokeza kuhusu wachezaji mpya kusajiliwa.

Eric Ten Hag Kocha wa Manchester United
Eric Ten Hag Kocha wa Manchester United
Image: HISANI

Meneja wa Manchester United Erik ten Hag amejibu tetesi zinazoendelea kuhusu yeye kuondoka katika klabu hiyo baada ya fainali za Kombe la FA mnamo Jumamosi, Mei 25.

Wakati akiwahutubia wanahabari siku ya Alhamisi, kocha huyo kutoka Uholanzi mwenye umri wa miaka 54 alidokeza kwamba kwa sasa anaangazia mchuano wa Jumamosi na sio kile kinachotokea baada ya hapo.

Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake katika Old Trafford, alikataa kutoa maoni lakini badala yake alidokeza kuhusu kuangazia miradi ya baadaye ya klabu.

"Ninazingatia tu kazi ninayopaswa kufanya na hiyo ni kushinda kwanza mchuano Jumamosi na kisha tuingie kwenye mradi. Kuendelea na mradi," Ten Hag alisema.

Aliongeza, "Nilikuja hapa kushinda mataji. Jumamosi, nina nafasi nyingine na tulifanikisha hili, tukapata nafasi hii kama timu na sasa lazima tuifikie."

Pia alizungumza kuhusu miradi inayoendelea katika klabu hiyo akidokeza kuhusu wachezaji mpya kusajiliwa na kupandishwa daraja kwa  baadhi ya wachezaji chipukizi.

“Wakati huo huo, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, bila shaka baada ya kila msimu mnapitia halafu tutaona tulipo kwenye mradi na mambo lazima tubadilike. Tulizungumza hivi majuzi juu yake. Chini kuna mambo mazuri sana - wachezaji wanaokuja, wachezaji wanaokua, dhamani zinakuja. Na, wakati huo huo, tunayo fursa kubwa Jumamosi kushinda kombe linalofuata," alisema.

Ten Hag amekuwa akikabiliwa na ukusoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki wa sok duniani kote kutokana na matokeo mabaya ya Man United katika msimu wa EPL uliomalizika wikendi iliyopita. Mashetani Wekundu walimaliza Ligi wakiwa nambari nane wakiwa na alama 60 pekee, na hivyo kuashiria kumaliza kwao kwa chini zaidi katika miaka mingi.

Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu meneja huyo wa Uholanzi tangu wakati huo huku baadhi ya ripoti zikisema kwamba anaweza kuondoka katika klabu hiyo baada ya fainali ya FA mnamo Mei 25.