Rooney asisitiza ndoto yake ni kufunza Man U au Everton, wiki 1 baada ya kuwa kocha wa Playmouth

"Ni ngumu kwa sababu nimekuwa nikisema kwamba ningependa kusimamia Everton au Manchester United," alisema kwenye The Overlap.

Kocha mpya wa Playmouth Argyle,Wayne Rooney amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba itakuwa "ndoto" yake kuinoa Manchester United katika siku zijazo.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza amerejea katika usimamizi baada ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu anayefuata wa Plymouth Argyle wiki iliyopita.

Jukumu hilo ni la kwanza kwa Rooney tangu alipotimuliwa Birmingham Januari baada ya utawala mbaya na wa muda mfupi uliodumu chini ya miezi mitatu na kupoteza michezo tisa kati ya 15 akiwa kwenye usukani wa timu iliyoshika nafasi ya sita alipofika lakini baadaye ilishuka daraja kutoka daraja la pili.

Kabla ya hapo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 aliwahi kuwa kocha wa Derby County na DC United inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka (MLS).

Rooney alikuwa na maisha mazuri ya uchezaji, akimaliza kama mfungaji bora wa muda wote wa England na Manchester United, na sasa ana ndoto ya siku moja kuchukua hatamu Old Trafford.

"Ni ngumu kwa sababu nimekuwa nikisema kwamba ningependa kusimamia Everton au Manchester United," alisema kwenye The Overlap.

"Labda ningesema United - hiyo ndiyo itakuwa kilele cha kuinoa Manchester United. Everton ingekuwa zaidi kutokana na mtazamo wa kihisia, klabu ninayoshabikia na kuipenda, lakini United wangekuwa kilele kwa kweli.”

Rooney alikuwa akifanya kazi kama mchambuzi wa televisheni kabla ya kuchukua mikoba ya Plymouth na ilikuwa inakisiwa kwamba angefuata taaluma hiyo badala yake.

Mshambulizi huyo wa zamani, hata hivyo, sasa amefichua jinsi ambavyo kila mara alitaka kurejea katika ukocha.

"Ni wazi nataka kurejea katika usimamizi," alisema Rooney, ambaye alikuwa akizungumza kabla ya kupata kazi ya Plymouth.

"Ni kitu ninachotaka kufanya na kujithibitisha. La mwisho, nilikatishwa tamaa na matokeo lakini pia jinsi yalivyoisha.”