Mfungaji bora kwenye AFCON, Emilio Nsue hakustahili kuchezea Equitorial Guinea, FIFA yasema

Nsue amepigwa marufuku ya miezi sita na shirikisho la soka la Equitorial Guinea (Feguifut) kutozwa faini ya Ksh 21.9 m.

Muhtasari

•Nsue aliwahi kuwakilisha timu za vijana chipukizi za Uhispania, ikiwemo katika Mashindano ya Uropa ya Vijana chini ya miaka 21.

•Desemba 2013, Fifa ilisema Nsue hastahili kuichezea Equitorial Guinea baada ya kuchezea timu za vijana za Uhispania kwenye mashindano rasmi.

Image: HISANI

FIFA imeamua kuwa mfungaji bora katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) takriban miezi mitano iliyopita, Emilio Nsue, hakuwahi kustahili kuichezea timu ya Equitorial Guinea katika kipindi chake chote cha miaka 11 ya uchezaji wa kimataifa.

Nsue aliwahi kuwakilisha timu za vijana chipukizi za Uhispania, ikiwemo katika Mashindano ya Uropa ya Vijana chini ya miaka 21.

Mnamo Desemba 2013, Fifa ilisema Nsue hastahili kuichezea Equitorial Guinea baada ya kuchezea timu za vijana za Uhispania kwenye mashindano rasmi, lakini aliendelea kuichezea nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Uchunguzi mpya ulianzishwa kuhusu kustahiki kwa Nsue mnamo Machi 2023, huku mshambuliaji huyo akipewa makataa ya siku sita kujibu.

Fifa ilisema: "Hakuna msimamo uliopokelewa kutoka kwa mhojiwa."

FIFA imeripotiwa kuchapisha uamuzi wa kina kueleza kwa nini mwezi uliopita, kamati yake ya nidhamu iliipokonya Equatorial Guinea ushindi mara mbili katika michezo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 iliyochezwa Novemba.

Katika michuano yote miwili, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 alifunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Namibia na Liberia lakini hakuwahi kupata kibali rasmi cha FIFA kuhama kutoka Uhispania kwenda Equatorial Guinea.

Nsue amepigwa marufuku kutojihusisha na soka la kimataifa kwa miezi sita na shirikisho la soka la Equitorial Guinea (Feguifut) kutozwa faini ya 150,000 pesa za Uswizi (Ksh 21.9 milioni).

Ilikuwa ni hukumu ya marudio ya hukumu za kinidhamu za FIFA za 2013 ambayo pia iliamuru Equatorial Guinea kutocheza mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2014 na kupoteza 3-0 kwa sababu Nsue hakustahili.

FIFA ilisema majaji wake wa nidhamu katika uchunguzi wa hivi majuzi zaidi walithibitisha sababu kutoka kwa kesi zinazohusiana na michezo ya 2013.

Majaji wa Fifa wamesema kuwa Nsue alipata tu uraia wa Equatoguinean (Machi 2013) baada ya kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa katika mashindano rasmi na Uhispania.