Antonio Conte amekabidhiwa jukumu la kufufua Napoli na kurudisha klabu hiyo kileleni mwa msimamo baada ya msimu mbaya.
Muitaliano huyo, ambaye atarejea kwenye uongozi baada ya mapumziko ya mwaka mmoja baada ya kuachana na klabu ya Tottenham Hotspur ya ligi kuu ya Uingereza, amesaini mkataba utakaomweka Stadio Diego Armando Maradona hadi 2027.
Conte atachukua jukumu la kuinoa timu ya Napoli ambayo ulinzi wake wa ubingwa ulidorora kabla ya mwisho wa msimu huu, huku klabu hiyo ikimaliza nafasi ya 10 na kushindwa kufuzu kwa mashindano ya Ulaya.
"Kwa hakika ninaweza kuahidi jambo moja nitafanya niwezavyo kwa ajili ya ukuaji wa timu na klabu. Ahadi yangu, pamoja na ile ya wafanyakazi wangu, itakuwa kamili," Conte alisema katika taarifa yake.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54, anajivunia uzoefu mkubwa katika Serie A, baada ya kutwaa mataji manne ya ligi akiwa kocha mkuu wa Inter Milan na Juventus.
Aidha alikuwa na mafanikio huko England akiwa na Chelsea, akishinda ligi kuu na kombe la FA akiwa na klabu hiyo ya London.
Napoli ilistahimili kampeni mbaya ya 2023-24, ikipitia mameneja watatu baada ya kocha Luciano Spalletti kuondoka na kuchukua kazi ya kocha mkuu wa Italia. Nafasi ya Spalletti ilichukuliwa na Rudi Garcia, ambaye alitimuliwa baada ya miezi minne msimu huu, kabla ya kocha wa zamani Walter Mazzarri kurejea kujaribu kubadilisha mambo.