Waandalizi wa mashindano ya kandanda ya kimataifa ya wanaume na wanawake wamekiri kuwa wanakabiliwa na "kibarua kigumu kupanga ratiba", lakini tarehe za matoleo yajayo zinakaribia kuafikiwa, BBC imeambiwa.
Wakati wa mahojiano nadra ya kina Veron Mosengo-Omba, katibu mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), aliahidi kwamba tangazo kuhusu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2024 nchini Morocco lingetolewa mwishoni mwa mwezi huu - akifichua kuwa kuna uwezekano mkubwa inaweza kubadilishwa hadi mwaka ujao.
"Tunastahili kucheza mwaka huu lakini tuna timu zinazoshiriki Olimpiki, kwa hivyo tunapaswa kutafuta tarehe nyingine," Mosengo-Omba alieleza BBC Michezo Afrika.
"Tunazungumza na Uefa, kwa sababu wachezaji wengi wanacheza Ulaya, Shirikisho la Vilabu la Ulaya na pia Fifa ili kupata tarehe inayofaa."
Wakati huo huo, Mosengo-Omba alithibitisha kwamba Caf inaweza kuandaa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, ambazo pia zitaandaliwa na Morocco, mapema 2026 kwa sababu ya muda wa Fifa wa Kombe la Dunia la Vilabu lenye timu 32 mwezi Juni na Julai mwaka ujao.
"Kwa wanaume, tunahitaji kuhakikisha kuwa tarehe ambazo tutakuwa tunachagua zitakuwa kwa maslahi ya wachezaji," alisema Mswizi huyo wa Kongo, akiangazia masuala yanayohusu mzigo wa wachezaji mashuhuri wa bara.
"Kwa hili tunahitaji kusawazisha vipengele tofauti na pia kujadili na washirika wetu kabala ya kuamua [tarehe] ya michuano hiyo. Kupanga ratiba ni kibarua kigumu kwa kila mtu.”