Pochettino avunja kimya baada ya kuondoka Chelsea

Meneja wa zamani wa chelsea,Mauricio Pochettino amesema kuwa alifurahishwa na kiwango ambacho timu ilifikia baada ya kuondoka.

Muhtasari

•Pochettino aliridhishwa na kiwango ambacho Chelsea ilifikia wakati wa usimamizi wake kama kocha mkuu wa klabu hio.

•Mkufunzi huyo wa zamani wa Chelsea atarejea ugani Stamford Bridge Jumapili hii kusimamia timu ya World XI Soccer Aid dhidi ya Uingereza.

Kocha Mauricio Pochettino
Gatty Images Kocha Mauricio Pochettino
Image: BBC Sport

Mauricio Pochettino amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuondoka Chelsea kabla ya kurejea Stamford Bridge Jumapili hii .

Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 52, aliihama Chelsea kwa makubaliano kati yake na wasimamizi wa klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa 2023/24, na kutoa nafasi kwa kocha mkuu mpya Enzo Maresca  ambaye alitangazwa rasmi kama mrithi wake Jumatatu 3,Juni 2024.

Pochettino alidokeza kuwa yeye na wafanyikazi wake wanaelewa jinsi klabu hiyo ilivyo muhimu kwa mashabiki na ndiyo maana wamefanya kazi kwa bidii ili kuwafurahisha. Mkufunzi huyo alionyesha kujivunia kiwango ambacho Chelsea ilifikia wakati wake.

"Nimefurahishwa sana na kiwango ambacho timu ilifikia na jinsi wachezaji na wafanyakazi wote wamefanya kazi kwa bidii ili kuongeza viwango vyao, wanastahili sifa kubwa..."

Aidha Pochettino pia ana imani kuwa kikosi hicho cha Chelsea chini ya mkufunzi mpya,Enzo Maresca kitafikia hatua ubora huku akiwatakia mafanikio mazuri msimu ujao.

"Nataka kuwatakia kila la kheri kwa msimu ujao..."Pochettino alidokeza.

Kufuatia mwanzo mbaya wa msimu ,Chelsea walikuwa washindi wa pili wa kombe la Carabao,wakafika nusu fainali ya FA  na kumaliza nafasi ya sita kwenye ligi ya primia baada ya kushinda mechi zao tano za mwisho za msimu huu.

Muda wa Pochettino kule Stamford Bridge bado haujaisha, kwani atarejea Jumapili kusimamia timu ya World XI Soccer Aid. Licha ya kuondoka Chelsea, Pochettino ameendelea kushikilia msimamo wake katika mchezo wa hisani, akiongoza kikosi kinachojumuisha nyota kama Eden Hazard na Usain Bolt.