Kwa nini Real Madrid haitashiriki Kombe la Dunia la vilabu 2025- Carlo Ancelotti

Ancelotti amesema kuwa Real Madrid haitakubali mwaliko kutoka FIFA wa kushiriki kombe la dunia la vilabu 2025

Muhtasari

•Kocha  huyo mwenye umri wa miaka 65 alisema kuwa wachezaji wake hawatashiriki katika mashindano hayo.

•Ancelotti amefichua kuwa kiasi ambacho FIFA itatoa kwa washindi ni kidogo mno ikilinganishwa na thamani ya mechi moja ya Real Madrid ambao ina thamani ya Euro milioni 20.

Carlo Ancelotti
Image: Hisani

Mkufunzi wa Real Madrid Carlo Ancelotti amesema kuwa Real Madrid haitakubali mwaliko wa FIFA wa kucheza Kombe la Dunia la Vilabu 2025.

Kombe la dunia la vilabu la FIFA lililopanuliwa kwa mara ya kwanza, likishirikisha vilabu 32 maarufu na ambalo litaandaliwa nchini Marekani, lina muda wa chini ya mwaka mmoja. Kati ya nafasi 32 za timu zinazoshindana, 29 zimejazwa na vilabu kutoka mashirikisho mbalimbali yakiwemo UEFA, CONMEBOL, CAF, AFC, OFC, na CONCACAF.

Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti la Italia Il Giornale siku ya Jumatatu, Ancelotti alifichua kuwa Madrid hawana mpango wa kushiriki. Kocha  huyo mwenye umri wa miaka 65 alisema kuwa wachezaji wake hawatashiriki katika mashindano hayo.

"Mechi moja ya  Real Madrid ina thamani ya Euro milioni 20, na FIFA wanataka kutupa kiasi hicho kwa mashindano yote...Kama sisi, vilabu vingine vitakataa mwaliko." Ancelotti alisema.

Aidha imefafanuliwa  na gazeti la The Athletic kwamba  klabu ya Madrid na FIFA wanadumisha uhusiano mzuri, na pande zote mbili zinawasiliana kuhusu kombe la dunia la klabu na masuala mengine.

Kombe la dunia la vilabu la FIFA lililoboreshwa ni mpango mkuu wa shirikisho la soka duniani, unaolenga kuiga mafanikio ya mashindano ya vilabu maarufu kama vile UEFA Champions League na Copa Libertadores.

Gazeti la The Athletic liliripoti kwamba FIFA haijatangaza miji itakayoandaa michuano hiyo, inayojulikana kama Mundial de Clubes FIFA 25.

Zaidi ya hayo, mikataba ya udhamini na thamani ya fedha kwa klabu zinazoshiriki bado inaendelea.Miongoni mwa klabu zilizojikatia tiketi  barani Ulaya ni: Real Madrid,Chelsea, Manchester City,Psg,Juventus,Salzburg,Porto,Intermilan,Benfica,Dortmund pamoja na Atletico Madrid.