Aliyekuwa mshambulizi wa Arsenal, Kevin Campbell afariki

Campbell alifunga mabao 148 katika mechi 542 akiwa na klabu nane katika maisha yake ya soka

Muhtasari

•Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Everton Kevin Campbell amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 54 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Image: HISANI

Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Everton Kevin Campbell amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 54 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Campbell alifunga mabao 148 katika mechi 542 akiwa na klabu nane katika maisha yake ya soka.

Alishinda mataji manne makubwa akiwa na Arsenal na pia alichezea Leyton Orient, Leicester, Nottingham Forest, Trabzonspor, Everton, West Brom na Cardiff.

Campbell alijitokeza mara ya mwisho kama mchezaji mnamo Februari 2007 kabla ya kuhamia kwenye utangazaji.

Everton ilisema mapema mwezi huu aliugua mwezi Mei na "alikuwa mgonjwa sana" hospitalini.

"Tumesikitika sana kujua kwamba mshambuliaji wetu wa zamani Kevin Campbell amefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi," Arsenal ilisema.

"Kevin alisifiwa na kila mtu kwenye klabu. Sote tunawafikiria marafiki na familia yake katika wakati huu mgumu. Pumzika kwa amani, Kevin."

Everton alisema: "Kila mtu katika Everton amehuzunishwa sana na kifo cha mshambuliaji wetu wa zamani Kevin Campbell akiwa na umri wa miaka 54 tu.

"Sio tu shujaa wa kweli wa Goodison Park na kielelezo cha mchezo wa Kiingereza, lakini mtu wa ajabu pia - mtu yeyote aliyewahi kukutana naye atajua. RIP, Super Kev."