Kombe la Euro 2024: Serbia yatishia kujitoa kutokana kitendo cha kuimbwa

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Serbia, Jovan Surbatovic, ametaka adhabu kali zaidi ichukuliwe.

Muhtasari
  • Sadiku alitoa ishara ya tai ya mikono miwili ya utaifa kuelekea mashabiki wa Serbia wakati wa mchezo dhidi ya Uingereza.

Serbia imetishia kujiondoa kwenye michuano ya Euro 2024 kutokana na kelele za nyimbo za mashabiki kwenye mechi kati ya Croatia na Albania siku ya Jumatano.

Mashabiki walisikika wakiimba kuhusu mauaji ya Waserbia wakati wa sare ya 2-2 kwenye mechi ya Kundi B.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Serbia, Jovan Surbatovic, ametaka adhabu kali zaidi ichukuliwe.

Aliliambia shirika la utangazaji la serikali la Serbia RTS: "Kilichotokea ni kashfa na tutaomba baraza la Uefa kuweka vikwazo, hata kama itamaanisha kutoendelea na mashindano."

Serbia wako Kundi C na walianza michuano hiyo kwa kuchapwa 1-0 na Uingereza siku ya Jumapili.

Surbatovic alisema kuwa "ana uhakika wataadhibiwa" kufuatia uamuzi wa Uefa siku ya Jumatano kufuta kitambulisho cha mwandishi wa habari wa Kosovar, Arlind Sadiku.

Sadiku alitoa ishara ya tai ya mikono miwili ya utaifa kuelekea mashabiki wa Serbia wakati wa mchezo dhidi ya Uingereza.

BBC imewasiliana na Serbia na Uefa kwa maoni zaidi. Serbia ilipigwa faini ya £12,250 baada ya mashabiki kurusha vitu wakati wa mechi ya Uingereza.

Serbia na Albania pia zilitozwa faini kutokana na mashabiki kutoka nchi zote mbili kuonesha mabango ya ramani za utaifa, nje katika mechi zao za ufunguzi.