Mabingwa mara ishirini na moja wa ligi kuu ya FKF, Gor Mahia wamepangwa katika kundi nzito kwenye michuano ya kombe la Kagame ya baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati (CECAFA).
Kwenye droo iliyofanyika Juni 2,jijini Dar es Salaam,Vinara hao wamepangwa Kundi B la michuano ijayo ya CECAFA Kagame Cup, inayoratibiwa kufanyika kati ya Julai 9 na Julai 21, 2024, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Timu hiyo itamenyana na washindi mara kumi wa ligi ya Sudan, Al Hilal , Red Arrows ya Zambia, na Telecom FC ya Djibouti.
Gor ilinyakua kombe hilo mwaka wa 1985 baada ya kuwashinda wapinzani wao wa kudumu wa ligi kuu AFC Leopards mabao 2-0 na kubeba Kombe lao la tatu la Kagame.
Baraka Kizuguto,ambaye ni mkurugenzi wa CECAFA alisema wanatarajia mashindano hayo yatakuwa na ushindani mkubwa kwani timu zitakuwa zikijiandaa na mashindano ya CAF yatakayoanza Agosti.
Mara ya mwisho michuano ya kanda hiyo ilipofanyika mwaka 2021 jijini Dar es Salaam, Express Fc ya Uganda iliifunga Nyasa Big Bullets FC kutoka Malawi bao 1-0.
Timu za juu kutoka kwa kila kundi na mshindi wa pili ataingia hatua ya nusu fainali.
Mechi hizo zitachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi na uwanja wa KMC uliopo Kinondoni.
Kundi A
Coastal Union (Tanzania),
Alwadi (Sudan),
JKU (Zanzibar),
Dekaheda FC (Somalia)
Kundi B:
Gor Mahia (Kenya),
Al Hilal (Sudan),
Red Arrows (Zambia),
Telecom FC (Djibouti)
Kundi C
Sports Club Villa (Uganda),
APR FC (Rwanda)
Singida Black Stars (Tanzania),
Al Mereik Bentui (Sudan Kusini)