Mechi mbili kubwa zilichezwa Ijumaa usiku huku nyingi zilizofuatwa Euro 2024 zikiingia katika hatua ya robo fainali.
Washindi wa Kombe la Dunia 2010, Uhispania walimenyana na wenyeji Ujerumani kwenye Uwanja wa MHPArena (Stuttgart) mwendo wa saa 7PM kwa saa za Afrika Mashariki huku washindi wa Euro 2016 Ureno wakimenyana na washindi wa Kombe la Dunia 2018, Ufaransa, kwenye Uwanja wa Volksparkstadion (Hamburg) saa 10 jioni. Mechi zote mbili zilipita muda wa kawaida kufuatia ubora wa wapinzani wote.
Katika mechi ya kwanza, wenyeji walinyamazishwa nyumbani na Uhispania kupata ushindi wa 2-1 baada ya muda wa ziada.
Kiungo wa RB Leipzig Dani Olmo aliifungia Uhispania bao la kwanza dakika ya 51 na kusaidia Mikel Merino wa Real Sociedad kufunga bao la pili dakika ya 119. Bao pekee la Ujerumani lilifungwa dakika ya 89 na kiungo wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz. Beki mwenye uzoefu Dani Carvajal wa Uhispania hata hivyo atakosa mechi ijayo kwani alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 120+5.
Ureno ilipambana vikali dhidi ya timu yenye nguvu ya Ufaransa lakini ilitolewa kwa mikwaju ya penalti. Hii ilikuwa baada ya timu zote mbili kuweza kufunga bao lolote katika muda wa kawaida pamoja na muda wa ziada.
Mshambulizi wa Atletico Madrid Joao Felix alishindwa kufunga penalti yake kwa Ureno huku Ufaransa ikifunga penalti zake zote tano.
Ufaransa sasa itamenyana na Uhispania katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa wiki ijayo.
Matokeo ya Ijumaa yalikuwa na maana kubwa kwa nyota wa Ujerumani Toni Kross na Thomas Muller kwani walikuwa tayari wamedokeza kuhusu kustaafu soka ya kimataifa. Wote wawili wana umri wa miaka 34 kwa sasa.
Pepe pia angeweza kuichezea Ureno mechi iliyopita kwa kuwa beki huyo mwenye umri wa miaka 41 alikuwa tayari amedokeza kuhusu kustaafu soka ya kimataifa.
Kuna madai kwamba nahodha wa Ureno Christiano Ronaldo pia angeweza kuichezea nchi yake mechi yake ya mwisho ya Euro kwani mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 39 huenda akastaafu hivi karibuni.
Jumamosi usiku, Uingereza itamenyana na Uswizi saa 7 mchana huku Uholanzi ikicheza na Uturuki saa 10 jioni katika siku ya pili ya robo fainali ya Euro 2024.