Harambee Stars huenda ikachezea nyumbani mechi za kufuzu Afcon -Nick Mwendwa

FKF ilifichua kuwa wataomba leseni ya muda kutoka kwa shirikisho la soka Afrika (Caf) ili kutumia uwanja wa Nyayo.

Muhtasari

•Nick Mwendwa alielezea matumaini kuwa serikali itakamilisha ukarabati wa uwanja wa Nyayo kwa wakati unaofaa.

• Kenya itaanza kampeni ya kufuzu kwa kombe la mataifa ya Afrika 2025 dhidi ya  Zimbabwe katika uwanja wa Nyayo mnamo Septemba 2,2024.

Wachezaji wa Harambee Stars
Image: facebook

Timu ya taifa ya kandanda ya wanaume Harambee Stars huenda ikacheza mechi zake za nyumbani katika uwanja wa Nyayo wakati wa kampeni ya kufuzu kwa kombe la mataifa ya Afrika 2025.

Rais wa shirikisho la soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa alisema watafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa kikosi cha Kenya kinachezea nyumbani.Hii inakuja muda mchache baada ya Kenya Kuchezea Malawi kwenye  mechi za kufuzu kwa kombe la dunia la 20

Stars ilitifuana vumbi na Burundi na Ivory Coast katika uwanja wa kitaifa wa Bingu mjini Lilongwe, Malawi kutokana na uhaba wa uwanja ulioidhinishwa na Fifa humu nchini.

Katika mahojiano,  FKF ilifichua kwamba wataomba leseni ya muda kutoka kwa shirikisho la soka Afrika (Caf) kutumia uwanja wa Nyayo kwa mechi za nyumbani za Stars katika mchujo wa mikondo miwili.

"Tuko katika harakati za kutuma maombi ya leseni ya muda mwezi huu na nina uhakika itatolewa," Mwendwa alisema.

Mwendwa alielezea matumaini kuwa serikali itakamilisha kituo cha michezo kwa wakati unaofaa.

"Ninataka kuwaahidi wakenya kwamba ikiwa waziri atamaliza kazi hiyo, tutaandaa mechi za kufuzu kwa Afcon nchini," akaongeza.

Kenya itaanza kampeni ya kufuzu kwa kombe la mataifa ya Afrika 2025 dhidi ya  Zimbabwe katika uwanja wa Nyayo mnamo Septemba 2. Mechi inayofuata ya Harambee Stars itakuwa dhidi ya Namibia mjini Windhoek mnamo Septemba 10.

Hii itafuatwa na pambano la mikondo miwili kati ya Kenya  na Cameroon mjini Yaounde mnamo Oktoba 7 kabla ya mchuano wa marudiano utakaofanyika Nairobi Oktoba 15.

Harambee Stars itamaliza kampeni yake dhidi ya Zimbabwe mjini Harare mnamo Novemba 11 kabla ya kumaliza udhia  na Namibia jijini Nairobi mnamo Novemba 19.

Timu mbili  katika kila kundi zinatarajiwa kufuzu kwa Afcon 2025 ,mashindano ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili.