Gor Mahia wateleza katika mechi ya ufunguzi ya kombe la Cecafa Kagame

Gor itachuana na Telkom FC kutoka Djibouti kwenye mechi yao ya pili

Muhtasari

•Gor Mahia ilipokea kichapo cha moja sifuri kutoka kwa Red Arrows Fc inayoshiriki ligi ya  Zambia kwenye mechi ya ufunguzi ya makundi , kombe la Kagame.

•Kwa sasa Al Hilal  kutoka Sudan inaongoza kundi B sawia na Red Arrows FC japo kwa wingi wa mabao.

Image: Facebook [Red Arrows fc ]

Mabingwa wa ligi kuu ya FKF, Gor Mahia walipokea kichapo cha 1-0  mikononi mwa  Red Arrows FC kutoka Zambia kwenye mechi ya ufunguzi ya kombe la  Cecafa Kagame Cup.

Licha ya kuonyesha  matumaini katika mchuano huo,mabingwa mara ishirini na moja wa ligi kuu ya FKF ,waliambulia patupu  kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi B uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam Jumatano usiku.

Kwenye mazungumzo na wanahabari baada ya mechi,kocha wa Gor Mahia Leonardo Martins Neiva amesema kuwa   hana wasiwasi na anahisi ilikuwa ni kwa wachezaji wake bado kujifunza anachotaka kutoka kwake, jambo ambalo anaamini litarekebishwa na wakati.

"Mchezo mgumu kwa timu zote mbili, katika kipindi cha kwanza timu kutoka Zambia ilidhibiti mchezo katika dakika 25 za kwanza lakini baada ya hapo, tulirekebisha mambo machache na kupata uwiano lakini kwa ujumla, walicheza vizuri zaidi yetu," Neiva alisema .

 Aliongeza; “Wakati wa mapumziko, tulirekebisha baadhi ya vitu na tuliporudi, tulikuwa na mpira na mzunguko lakini ni mchezo wa kwanza kwangu, hawanijui, hivyo tunahitaji muda zaidi kuweka pamoja masuala yetu ya kiufundi na kimwili.

Gor itakuwa inajaribu kufufuwa matumaini yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Telkom Fc kutoka Djibouti kabla ya kumaliza mechi ya makundi dhidi ya Al Hilal.

Kwa sasa Al Hilal inaongoza kundi B kwa alama tatu,sawia na Red Arrows FC japo wana wingi wa mabao.