Gor Mahia kulenga kombe la kimataifa la Coal City baada ya kutolewa kwenye 'Kagame Cup'

Gor itachuana dhidi ya vinara wa Brazil Sport Club Corinthians Paulista mnamo Agosti 2, mjini Enugu, Nigeria.

Muhtasari

•Gor Mahia walishindwa kupata ushindi wowote tangu mashindano ya kombe la Kagame la Cecafa kung'oa nanga.

•Walipoteza 1-0 dhidi ya Red Arrows Fc,sare ya 1-1  na Telkom Fc kutoka Djibouti kabla ya kupoteza 2-0 mikononi mwa Al Hilal kutoka Sudan.

Image: FACEBOOK//GOR MAHIA

Mabingwa mara ishirini na moja  wa ligi kuu ya Kenya, Gor Mahia waliondolewa kwenye mashindano ya kombe la Kagame la Cecafa bila ushindi wowote.

Gor Mahia walianza michuano hio kwa kufungwa 1-0 na Red Arrows ya Zambia na kufuatiwa na sare ya 1-1 dhidi ya Telkom FC kutoka Djibouti, jambo lililokatiza matumaini yao ya kufuzu kwa raundi inayofuata.

Matumaini ya Gor yalififia kwani ,michuano hiyo ilikuwa na  timu 12 zilizogawanywa katika vikundi vitatu, huku timu zitakazomaliza kwenye nafasi ya kwanza   na mshindi wa  nafasi ya pili bora akifuzu kwa nusu fainali.

Hata hivyo  SC Villa kutoka Uganda iliwapiku Gor kwani walikuwa na pointi 5  katika Kundi C wakiwa na nafasi bora ya kumaliza  katika nafasi ya pili bora kabla ya mechi ya mwisho.Gor Mahia wangemaliza kwa alama 4 ikiwa wangepiga Al Hilal.

Mechi ya mwisho ya Gor Mahia iliishia kwa kushindwa 2-0 na Al Hilal kutoka Sudan na kufunika kabisa matumaini yao.

Gor Mahia sasa  wanatazamiwa kufungua kampeni zao kwenye kombe la kimataifa la Coal City dhidi ya vinara wa Brazil Sport Club Corinthians Paulista mnamo Agosti 2, mjini Enugu, Nigeria.

Michuano hiyo iliyoandaliwa na serikali ya jimbo la Enugu, itaanza Agosti 1 hadi Agosti 11, ikishirikisha klabu maarufu kutoka Nigeria na timu nyingine za kimataifa.

Ratiba ya Gor Mahia imethibitishwa, na baada ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Corinthians, itamenyana na Remo Stars ya Jimbo la Ogun mnamo Agosti 4, ikifuatiwa na pambano dhidi ya Kano Pillars mnamo Agosti 6.

Baada ya kombe hilo, wataelekeza nguvu zao tena  kwenye hatua ya awali ya ligi ya mabingwa Afrika, ambapo watamenyana na El Merreikh kutoka Sudan Kusini Agosti 23.

Iwapo watashinda, watakutana na Al Ahly kutoka Misri ambao wameeka rekodi nzuri katika mashindano hayo.