Kiungo anayechipukia wa Junior Starlets,Marion Serenge ameshinda tuzo ya LG/SJAK ya mwanaspoti bora wa mwezi wa Juni.
Hii inafuatia uchezaji wake mzuri katika mechi za kufuzu kwa kombe la dunia la FIFA la wanawake wasiozidi umri wa miaka 17.
Juhudi zake katika mechi ya mikondo miwili dhidi ya Burundi ziliwafanya warembo hao wa Kenya kuwa timu ya kwanza ya kenya kufuzu kwa kombe la dunia, kwa jumla ya mabao 5-0.
"Napenda kuwashukuru makocha wangu, wachezaji wenzangu na mashabiki wetu wote kwa sapoti, bila wao ningeshinda tuzo na Starlets isingefuzu kombe la dunia," alisema Serenge.
Serenge ambaye ndiye mwanamichezo mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kushinda tuzo hiyo, alibeba kombe la kipekee na mashine ya kufulia ya LG.
Mwanafunzi huyo wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Archbishop Njenga Girls alimshinda bingwa wa Afrika Alexandra Ndolo, miongoni mwa walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ya kila mwezi.
Ndolo alicheza vyema katika mashindano ya uzio wa Afrika huko Casablanca, Morocco ambapo alishinda dhahabu katika kitengo cha wanawake wakuu mnamo Juni 7, 2024.
Kipa wa Junior Starlets, Velma Abwire, nahodha wa timu ya Shujaa Vincent Onyala, Emmanuel Wanyonyi mshindi wa medali ya fedha ya dunia katika mbio za mita 800, mshambuliaji wa Gor Mahia Benson Omalla, kipa wa Kenya Police fc Patrick Matasi, Zeddy Cheruiyot na Sarah Wasike pia waliteuliwa.