Kocha mkuu wa klabu ya Manchester United,Eric ten Hag amedokeza kuwa bado yupo katika harakati za kujenga kikosi chake.
Raia huyo wa Uholanzi amesema kuwa kikosi chake kina wachezaji wachache ukilinganisha na timu zingine huku akilaumu majeraha kwa kumaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita.
Ten Hag mapema mwezi huu aliongeza kandarasi yake hadi 2026 licha ya uvumi kwamba angeondoka baada ya msimu mbaya kando na kushinda kombe la FA mwishoni mwa kampeni.
Kwenye mazungumzo Ijumaa na gazeti la kila siku la Uholanzi Algemeen Dagblad, Ten Hag alitaja jumla ya mechi 61 za klabu yake katika mashindano yote msimu uliopita kuwa "za ajabu tu".
“Sisi sio timu pekee iliyokabiliwa na majeraha, vilabu vingine vilikuwa na hali kama hiyo. Msimu uliopita tulikuwa na majeruhi mara kwa mara kwa wachezaji katika nafasi sawa, wote nyuma. Wakati fulani tulikuwa karibu hakuna mabeki."
Aliongeza; "Nilipoanza hapa, United ilikuwa haijashinda kombe kwa miaka sita na haikuwa hivyo kwa sababu hawakuwa na wasimamizi wazuri hapa. Hii ina maana kuwa utunzi na ubora wa kikundi cha wachezaji unachangia pakubwa."
United imekuwa ikifanya usajili wa kupendeza baada ya kumsajili beki chipukizi wa Ufaransa ,Leny Yoro, kutoka Lille OSC.Beki huyo wa Ufaransa ametia saini kandarasi hadi Juni 2029, akiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Kwa sasa wapo katika harakati ya kumsaini kiungo wa Psg , Manuel Ugarte huku kukiwa na madai pia ya kumchukua beki wa Bayern Munich na raia wa Uholanzi Matthijs De Ligt.