Mkufunzi wa Manchester United Erik ten Hag anasema kocha wa zamani wa muda Ralf Rangnick alikuwa "sahihi kabisa" kuhusu klabu hiyo kufanyiwa "mabadiliko makubwa".
Ten Hag, 54, aliteuliwa kuwa kocha mnamo 2022 baada ya Rangnick kushikilia hatamu kwa miezi saba.
Mjerumani huyo, ambaye sasa anainoa Austria, aliiongoza United hadi nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya England lakini alishinda mechi 11 pekee kati ya 29 alizocheza.
Rangnick alihitimisha kuwa klabu ilihitaji upasuaji wa "moyo" na kwamba matatizo yake hayangeweza kutatuliwa kupitia "mabadiliko madogo".
Ten Hag, ambaye alitia saini nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja mwezi huu, anasema uchambuzi wa Rangnick ulikuwa sahihi.
"Rangnick alikuwa sahihi kabisa," Ten Hag alisema katika mahojiano na gazeti la Uholanzi AD Sportwereld.
"Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kushughulikia hili kwa miaka miwili, lakini alisema ni sawa kabisa: ni operesheni ya kina, ngumu sana. Na nilijua nilipoanza kuwa itakuwa kazi ngumu." alisema.
United wamefanyiwa mabadiliko makubwa nje ya uwanja tangu Sir Jim Ratcliffe apate asilimia 27.7 ya hisa za klabu hiyo Desemba mwaka jana.
Omar Berrada, Dan Ashworth, Jason Wilcox na Christopher Vivell wote wamejiunga katika nyadhifa za ngazi ya bodi mwaka huu, wakati klabu imetoa £50m kuboresha uwanja wa mazoezi.
Mshambuliaji Joshua Zirkzee na mlinzi Leny Yoro wamejiunga na klabu hiyo Bologna na Lille mtawalia katika wiki moja iliyopita, huku Ten Hag akithibitisha kuwa anamsaka beki wa Bayern Munich na Uholanzi Matthijs de Ligt.