Nahodha wa Chelsea Reece James apata jeraha lingine miezi 3 baada ya kurejea uwanjani

James amepata jeraha jingine, siku chache tu kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Muhtasari

•Beki huyo mwenye umri wa miaka 24 alipata jeraha dogo la misuli ya paja wiki iliyopita, wakati maandalizi ya msimu mpya yakiendelea.

•Msimu uliopita, alirejea uwanjani mwezi Mei, kuelekea mwisho wa msimu baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi Desemba.

Reece James kuwa nje hadi Machi.
Reece James kuwa nje hadi Machi.
Image: CHELSEA

Nahodha wa klabu ya Chelsea, Reece James amepata jeraha jingine, siku chache tu kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Ripoti kutoka Uingereza zinaonyesha kuwa beki huyo mwenye umri wa miaka 24 alipata jeraha dogo la misuli ya paja wiki iliyopita, wakati maandalizi ya msimu mpya yakiendelea.

Habari njema ni kwamba jeraha hilo limeripotiwa kuwa si mbaya sana, lakini wahudumu wa afya wa Chelsea watakuwa makini ili kumrejesha katika hali nzuri zaidi kabla ya kurejea tena uwanjani.

Miaka ya hivi majuzi  haijakuwa rahisi kwa beki huyo wa kushoto wa miaka 24, mwenye kipaji sana.  Katika ki[indi hicho, amekumbwa na majeraha kadhaa mabaya, napia amepigwa marufuku ya kucheza mara nyingi, na hivyo kuathiri muda wake wa kucheza.

Msimu uliopita, alirejea uwanjani mwezi Mei, kuelekea mwisho wa msimu baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi Desemba.

James alikuwa amecheza kwa dakika 27 pekee wakati wa mechi ya Chelsea dhidi ya Everton mnamo Desemba 12 kabla ya kutolewa nje baada ya jeraha la mguu alilopata kumfanya ashindwe kuendelea kucheza.

Katika taarifa yake wiki mbili baadaye, beki huyo mwenye umri wa miaka 24 alifichua kwamba alifanyiwa upasuaji ili kurekebisha kabisa tatizo ambalo lilikuwa likijirudia katika miezi iliyopita na kumfanya ashindwe kucheza.

"Ulimwengu wa kandanda ulijua nilijeruhiwa lakini utaratibu ambao ningefanya wakati huu ulichukua muda mrefu zaidi kupata suluhisho bora," Reece James alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram .

Aliambatanisha taarifa yake na picha yake akiwa amelazwa kwenye kitanda cha hospitali huku akiinua kidole gumba chake cha kushoto kuashiria anaendelea vizuri.

"Nilifanyiwa upasuaji  ili kujaribu kurekebisha tatizo langu la misuli ya paja lililokuwa linajirudia, afueni imeanza, kimwili na kiakili," aliongeza.

Mwanasoka huyo wa Kimataifa wa Uingereza aliendelea kulalamika kuhusu mashambulio na chuki alizopokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya kupata jeraha tena.

"Tangu jeraha hili nimekuwa na usaidizi mzuri lakini kikubwa zaidi ni chuki na mashambulio. Niamini, sitaki kujeruhiwa. Nina furaha zaidi ninapocheza soka," alisema.

Aliongeza, "Shukrani kwa watu wanaoelewa ambao wananiunga mkono licha ya hali ya juu au ya chini, inaenda mbali".