Beki wa Man Utd Lisandro Martinez aeleza kwanini ‘alimnyonga’ Amada Traore wa Fulham

“Nililazimika kumtuma kurudi gym. Nilijifunza kutoka hali ya kwanza ambapo yeye alianza ‘kuninyonga’, hivyo ikabidi ‘nimnyonge’ pia,” alisema.

Muhtasari

• Martinez alianza pamoja na Harry Maguire katika safu ya ulinzi ya kati, huku United ikikosa usajili wa majira ya kiangazi Leny Yoro kutokana na jeraha.

LISANDRO VS TRAORE.
LISANDRO VS TRAORE.
Image: HISANI

Beki wa Manchester United, Muargentina Lisandro Martinez amefunguka kuhusu mzozo uliotokota baina yake na winga wa Fulham Adama Traore katika mechi ya ufunguzi ya ligi ya premia Ijumaa usiku baina ya timu hizo mbili.

Beki huyo alizungumza na Sky Sports baada ya mechi na kutania kwamba alilazimika kumtuma Traore kurudi kwenye gym, baada ya kuonekana kupapurana na kuangushana kwenye zulia la kijani ugani Old Trafford.

Martinez hata hivyo aliweka wazi kwamba Traore ndiye alianza kumnyonga naye ikabidi ajibu mipigo iliyomtuma kurudi kwenye gym.

“Nililazimika kumtuma kurudi gym. Nilijifunza kutoka hali ya kwanza ambapo yeye alianza ‘kuninyonga’, hivyo ikabidi ‘nimnyonge’ pia,” alisema.

Joshua Zirkzee alifunga bao la ndoto kwenye mechi yake ya kwanza huku vijana wa Erik ten Hag wakiambulia pointi tatu za mwishoni kwenye uwanja wa Old Trafford na kuanza kampeni ya Ligi Kuu kwa ushindi.

Martinez alianza pamoja na Harry Maguire katika safu ya ulinzi ya kati, huku United ikikosa usajili wa majira ya kiangazi Leny Yoro kutokana na jeraha na mchezaji mwenzake mpya Matthijs De Ligt kwenye benchi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina aliulizwa maswali na Traore katika hatua za mwanzo kabla ya kumalizana na Mhispania huyo, na kumnyang'anya mpira wakati akikimbia kwenye eneo la hatari na kusababisha nyota huyo wa Fulham kuanguka chini.

United wataendelea na kampeni zao ugenini dhidi ya Brighton Jumamosi ijayo kabla ya kumenyana na Liverpool katika uwanja wa Old Trafford Jumapili ya Septemba 1.