Sancho awataja Drogba na Lampard kama mifano bora iliyomvutia kujiunga na Chelsea

"Mifano yangu bora walikuwa Didier Drogba na Frank Lampard na sasa nina nafasi ya kuchezea klabu hii kama wao. Ni hisia kubwa," Sancho alisema kwa furaha.

Muhtasari

• Sancho alijiunga na klabu hiyo ya London Magharibi kwa mkopo akitokea Manchester United.

• Alisema kwamba alivutiwa na wazo la kurudi jijini London, eneo ambalo alisema alikulia maisha yake mengi ya utotoni.

Jadon Sancho
Jadon Sancho
Image: Chelsea TV

Winga Jadon Sancho katika mahojiano yake ya kwanza kama mchezaji wa Chelsea amefunguka kulichomvutia kujiunga na The Blues.

Sancho alijiunga na klabu hiyo ya London Magharibi kwa mkopo akitokea Manchester United.

Alisema kwamba alivutiwa na wazo la kurudi jijini London, eneo ambalo alisema alikulia maisha yake mengi ya utotoni.

Pia alifichua kwamba alikuwa anashabikia Chelsea akiwa mtoto na kuwataja magwiji Frank Lampard na Didier Drogba kama mifano bora ya Chelsea iliyomvutia kutaka kuandikisha historia kama wao kwenye jezi ya samawati.

"Chelsea ni klabu yenye historia kubwa. Mifano yangu bora walikuwa Didier Drogba na Frank Lampard na sasa nina nafasi ya kuchezea klabu hii kama wao. Ni hisia kubwa," Sancho alisema kwa furaha.

Akizungumzia ushawishi wa kujiunga na Chelsea, Sancho alimsifia kocha Enzo Maresca kama mtu ambaye alimpigia simu na kumuelezea moja kwa moja jinsi atamfanya kuwa wa maana katika kikosi cha Chelsea na pia kumfanya kurejesha fomu yake ya awali kabla kujiunga na Man Utd.

"Nadhani ni meneja ndiye aliyenivutia sana kwenye mradi," Sancho alielezea.

"Nilimfahamu tangu akiwa na Pep Guardiola pale Manchester City. Alizungumza nami kwa simu kuhusu mradi huu na kile alichokuwa akijenga hapa, na kwa mchezaji mchanga kama mimi inasisimua na siwezi kusubiri kuanza."

Anaamini mtindo wa soka wa Maresca unafaa kwake.

Alisema: "Wananisajili kwa sababu na kuchangia timu, na niko tayari kufanya hivyo. Nafurahia ukufunzi wake. Mawinga wanapoingia kwenye mpira, yeye huwapenda kwenda moja dhidi ya moja na kuwa moja kwa moja. Tunacheza mechi nyingi za moja-mbili na 10s na mchanganyiko wa mshambuliaji hucheza. Inavutia sana na ni mtindo ninaocheza."