Nahodha wa Gor Mahia Philemon Otieno amesema wako tayari kutwaa ushindi katika mechi kali ya Dabi ya Mashemeji linalosubiriwa kwa hamu ugani Nyayo Jumapili.
AFC Leopards watakuwa wenyeji wa wapinzani wao hao wa jadi katika mchuano huo wa 96 wa dabi hiyo inayofuatiliwa pakubwa.
K'Ogalo inaingia uwanjani bila kocha mkuu baada ya Mbrazil Leonardo Neiva kutimuliwa wiki jana kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha yaliyopelekea mashabiki kumtaka ajiuzulu.
Hata hivyo, Otieno anaamini mabingwa hao mara 21 wa Kenya bado wanaweza kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao wakubwa licha ya kutokuwa na kocha.
"Nataka kuwahakikishia wafuasi wetu tunafanya kila tuwezalo kuandikisha matokeo chanya kwenye Mashemeji derby," Otieno alisema.
"Tunataka wawe na subira na sisi, na tutahakikisha tunapata matokeo chanya kufikia tarehe 24," aliongeza.
Otieno alisema yeye na wachezaji wenzake wanaelewa jinsi mchezo huo ulivyo muhimu kwa wafuasi wao waliojitolea.
"Ni mchezo mkubwa kwetu kama timu na pia kwa nchi. Kwa hivyo, tuko tayari kama timu, na maandalizi yanaendelea vizuri.
Tunatazamia mchezo mzuri tarehe 24. Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa tunapata matokeo chanya,” alihitimisha.