Kazi ya kocha Engin Firat huenda ikafika kikomo baada ya timu ya taifa la Kenya Harambee Stars kukosa kufuzu kombe ya mataifa barani Afrika AFCON ya mwaka 2025.
Kocha huyo baada ya mechi ya mwisho ya kundi J iliyochezwa nchini Afrika Kusini ambapo Harambee Stars ilitoka sare ya kutofungana na Namibia, aliekekea Uturuki taifa anakotoka huku wachezaji wakirejea nchini Jumatano jioni.
Akizungumza mnamo Jumatano, waziri wa michezo Kipchumba Murkomen alidokeza kuwa kulikuwepo na makubaliano baina ya kocha huyo na shirikisho la soka nchini kuwa ikiwa Kenya haitafuzu kushiriki AFCON ya 2025 nchini Morocco, mkataba wa kocha huyo kuendelea kuiongoza timu ya taifa la Kenya, itasitishwa.
“Nafahamu kuhusu makubaliano baina ya FKF na kocha, ambayo yanabainisha kuwa kushindwa kufuzu kwa Kenya kushiriki AFCON, kungesababisha kukatikakwa mkataba.” Alisema Murkomen.
Kwa mujibu wa Murkomen, mkataba wa Firat na FKF utasitishwa kufuatia makubaliano yaliyoafikiwa na mbayo wizara ya michezo ndio ilikuwa mdhamini wa mkataba huo.
“Kwa kuwa wizara ilifadhili mkataba huo, kwa kuzingatia kushindwa kwetu kukidhi sifa, tutaheshimu sehemu hiyo ya makubaliano ya ksitisha utoaji wa rasilimali zaidi.” Alisema Murkomen.
Akielekea
Uturuki baada ya mechi ya mwisho ya Harambee Stars nchini Afrika Kusini, kocha
Firat alidokeza kuwa angerejea nchini Kenya kuendelea na matayarisho ya timu ya taifa kushiriki
kipute cha CHAN mwakani.