logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kenya Police FC yatimua benchi la ufundi

Beldine Odemba ameteuliwa kuwa kocha mkuu kwa muda.

image
na Tony Mballa

Football21 November 2024 - 11:32

Muhtasari


  • Polisi, ambao walimaliza wa tatu katika msimu uliotangulia, wamefanikiwa kusajili ushindi mmoja pekee.
  • Wamecheza sare tatu na kupoteza moja, matokeo hayo yakiwaacha katika nafasi ya 15 kwenye jedwali la ligi.

Benchi la ufundi la Kenya Police



Klabu ya Ligi Kuu ya Kenya, Police FC, imetimua benchi zima la ufundi linaloongozwa na Salim Babu siku chache baada ya Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo Chris Onguso kulalamika kuhusu msusuru wa matokeo duni.

Beldine Odemba anayeongoza timu ya wanawake, Kenya Police Bullets, ameteuliwa kuwa kocha mkuu kwa muda.

Haya yanajiri wakati ambapo timu hiyo inatatizika kuandikisha matokeo mazuri msimu huu.

Polisi, ambao walimaliza wa tatu katika msimu uliotangulia, wamefanikiwa kusajili ushindi mmoja pekee.

Wamecheza sare tatu na kupoteza moja, matokeo hayo yakiwaacha katika nafasi ya 15 kwenye jedwali la ligi.

Awali, aliyekuwa kocha mkuu wa Ulinzi Anthony Kimani aliletwa kuinoa timu hiyo wakati wa michuano ya Kombe la Mashirikisho ya Caf baada ya kubainika kuwa Babu hakuwa na Leseni A ya CAF.

Klabu hiyo iliwakilisha Kenya katika Kombe la Shirikisho la CAF msimu uliopita, na walitolewa katika raundi ya pili ya awali baada ya kuangukia kwa vigogo wa Misri Zamalek SC.

Odemba ataiongoza timu hiyo katika mechi ijayo dhidi ya Kariobangi Sharks huku klabu hiyo ikitafuta mbadala wake wa kudumu, unaotarajiwa kutangazwa wiki ijayo.

Anakuwa kocha wa pili wa kike kuongoza timu ya Ligi Kuu ya Kenya ya wanaume, akifuata nyayo za Jackline Juma wa FC Talanta.

Klabu hiyo hapo awali iliwaajiri Francis Baraza na Mcroatia Zdravko Logarusic kama makocha wakuu.

Chini ya uongozi wa Babu, timu hiyo ilimaliza vyema msimu uliopita, na kushinda Kombe la FKF baada ya kuwalaza KCB katika fainali ya kufuzu kwa Kombe la Shirikisho la CAF.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved