Mshambulizi wa timu ya taifa la Kenya kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 Valarie Nekesa, ameteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji chipukizi wa mwaka barani Afrika katika tuzo za CAF za mwaka 2024.
Mchezaji huyo alifungia Junior Starlets bao la kwanza la Kenya katika mashindano ya kombe la dunia yalioandaliwa nchini Dominican katika mechi dhidi ya Mexico. Mechi hiyo, Junior Starlets walishinda kwa mabao mawili kwa moja ushindi ambao uliwaweka katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la kundi C.
Nekesa, mwanafunzi wa Madira Girls anatarajia ushindani mkali kutoka kwa wachezaji wengine chipukizi barani Afrika ikiwemo Chiamaka Okwuchukwu na Flourish Sebastian kutoka Nigeria ambao pia walishiriki kombe ya dunia.
Katika tuzo hizo za mwaka 2024, kocha wa Junior Starlets Mildred Cheche pia ameteuliwa kuwania tuzo ya kocha wa mwaka kwa timu za wanawake barani Afrika. Katika tuzo hizo, Mildred Cheche wa Junior Starlets, Lamia Boumehdi wa TP Mazembe na Mbayang Thiam wa Algiers De La Medina ndio makocha wa kike wanaofunza timu za kike watakaowania tuzo hiyo.
Mbali na Mildred Cheche na Valarie Nekesa kutoka Kenya
kujumuishwa kwenye tuzo hizo, timu ya taifa la Kenya ya wasichana wasiozidi
umri wa miaka 17, pia imejumuishwa kwenye tuzo za timu ya taifa ya mwaka 2024.