logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Aliyekuwa meneja wa muda wa Man United Ruud van Nistelrooy kurejea EPL kama kocha wa Leicester

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Steve Cooper kutimuliwa baada ya kuwa meneja wa Leicester kwa siku 157.

image
na Samuel Mainajournalist

Football28 November 2024 - 07:29

Muhtasari


  • Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 48 anaripotiwa kuwa anayependekezwa kuchukua nafasi ya Steve Cooper.
  • Uteuzi wa Van Nistelrooy unakuja wiki mbili baada ya kuacha nafasi yake kama kocha wa muda wa Man United


Aliyekuwa meneja wa muda wa Manchester United Ruud van Nistelrooy yuko tayari kurejea kwa ghafla katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 48 anaripotiwa kuwa anayependekezwa kuchukua nafasi ya Steve Cooper kama meneja mpya wa Leicester City.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Steve Cooper kutimuliwa baada ya kuwa meneja wa Leicester kwa siku 157. Haya yalitokea baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Chelsea Jumamosi kwenye Ligi ya Premia.

Uteuzi wa Van Nistelrooy unakuja wiki mbili baada ya kuacha nafasi yake kama kocha mkuu wa muda katika klabu ya Manchester United, akichukua mikoba ya Erik ten Hag ambaye alitimuliwa.

Katika Man United, Van Nistelrooy alisimamia ushindi mara tatu na sare moja wakati wa kipindi chake kidogo kama meneja.

Hata hivyo aliondoka mapema mwezi huu baada ya kuambiwa hatapewa jukumu katika wahudumu wa ofisi ya meneja mpya Ruben Amorim.

Ushindi mara mbili wa Van Nistelrooy ulikuwa dhidi ya Leicester, ushindi wa 5-2 katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Carabao na ushindi wa 3-0 kwenye Premier League mapema mwezi huu.

Mshambulizi huyo wa zamani wa Manchester United na Uholanzi atajiunga na Foxes na klabu hiyo katika nafasi ya 16 kwenye Ligi ya Premia baada ya michezo 12 na pointi moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja.

Cooper aliajiriwa msimu huu wa joto kuchukua nafasi ya Enzo Maresca baada ya Muitaliano huyo kujiunga na Chelsea, lakini alishinda mechi mbili pekee za Premier League.

Jukumu pekee la awali la Van Nistelrooy kusimamia timu ya wakubwa ilikuwa msimu wa kuinoa PSV mnamo 2022-23 ambapo alishinda Kombe la Uholanzi, kabla ya kujiunga na United kama kocha msaidizi mnamo Julai.

Mechi inayofuata ya Leicester itakuwa ugenini dhidi ya Brentford siku ya Jumamosi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza na ingawa haijafahamika iwapo Van Nistelrooy atakuwa dimbani, ukaribu wa wikendi unamaanisha kuwa hakuna uwezekano wa kuchukua jukumu la kuinoa timu hiyo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved