Wawaniaji wa urais wa shirikisho la soka nchini FKF Hussein Mohamed na mwenzake McDonald Mariga wamepata uungwaji mkono kutoka kwa seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago.
Hussein na Mariga waliidhinishwa kuwania urais wa FKF na bodi ya uchaguzi ya shirikisho hilo katika uchaguzi ambao umeratibiwa kuandaliwa mnamo Disemba 7, 2024 utakaoshirikisha wapiga kura 94 ambao ni wawakilishi na vilabu na wenyekiti wa matawi 48 waliopigiwa kura katika hatua ya kwanza ya mchakato wa upigaji kura katika katiba ya FKF kipengee cha uchaguzi.
Kupitia kurasa zao kwenye jukwaa la X, wamechapisha video ya seneta Mandago akizungumza katika mkutano kuwa wawili hao ndio wanaweza kuimarisha na kusimamia soka ya Kenya kwa njia inayostahili.
Akizungumza katika mkutano huo, seneta Mandago amesema kwamba wakati umefika wa mashirikisho ya smichezo nchini kuongozwa na watu ambao walikuwa wachezaji katika michezo husika.
“Wakati tuna haya mashirikisho, wacha tuwe na viongozi wanaoendesha mashirikisho hayo waliowahi kushiriki katika michezo hiyo. Hakuna haja ya kuokota mtu kama mimi nilikuwa nachoma makaa naambiwa simamia kandanda.” Alisema seneta Jackson Mandago.
Kwa mujibu wa Mandago, amesema kuwa kandanda itakuwa bora ikiwa uongozi wa shirikisho utakuwa na Mariga pamoja na Hussein ambao walishiriki katika soka.
Mandago
alisema kuwa tofauti ya mashirikisho yanayofanya kazi vyema na yale
yanayoboronga ni kuwa mashirikisho yanayosuasua ni yale ambayo uongozi wake
unaendeshwa na watu wasio na haja katika michezo ila wako kileleta mwa
mashirikisho hayo kwa ajili ya mambo yao binafsi.