Aliyekuwa mchezaji wa Nairobi City Stars na Mathare United Lennox Ogutu ameondolewa marufuku ya kutoshiriki kabumbu baada ya kesi iliyokuwa ikimkabili kufutiliwa mbali na mahakama ya kusuluhisha mizozo ya michezo (CAS) ya Uswisi.
Mchezaji huyo wa safu ya ulinzi, alikumbwa na kesi ya madai ya kuhusika na upangaji wa mechi maarufu kama match fixing akiwa katika klabu ya Mathare United mnamo mwaka wa 2023.
Kesi hiyo imetupiliwa mbali baada ya mchezaji huyo kwa ushirikiano na chama cha soka cha Kenya KEFWA, kupinga marufuku yaliyokuwa yamewekwa kwake kwa mafanikio.
Kutokana na kushinda kesi hiyo, mchezaji huyo sasa yuko huru kujiunga na timu yoyote ya kabumbu nchini Kenya baada ya shirikisho la Kenya nchini FKF kuondoa marufuku dhidi yake.
Katika barua ya KEFWA, wameishukuru mahakama ya kusuluhisha migogoro ya michezo ya CAS, kwa kuiangazia kesi hiyo kwa haki. Uamuzi huo wa CAS, sasa unamweka Ogutu katika nafasi nzuri ya kucheza sokakitaaluma bilaya kuwekewa vikwazo.
Vile vile, KEFWA imewashukuru washikadau wote waliohusika katika kuhakikisha kuwa mchezaji huyo anapata haki na hatimaye anarejea kusakata boli.
Aidha KEFWA imeomba FKF kuweka kipaombele mchakato wa
kusuluhisha kesi zinazowakabili wachezaji ikisema kuwa takribani wachezaji 30
wa kabumbu wamesimamishwa kushiriki michezo licha ya kesi zinazowakumbuka
kukosa kusikilizwa.