Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula ameahidi kuisadia timu ya Nzoia Sugar FC katika ligi ya kitaifa nchini ili kurejea kwenye ligi kuu ya soka nchini katika msimu ujao.
Wetang’ula amsema hayo mnamo Alhamisi asubuhi alipokutana na usimamizi wa klabu hiyo ukiongozwa na mwenyekiti Evans Kadenge, mwana wa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa kabumbu Joe Kadenge.
Nzoia Sugar FC ilishushwa daraja kutoka ligi kuu nchini FKFPL baada ya kukosa kujikakamua kuandikisha matokeo mazuri msimu jana.
Katika kuisadia klabu hiyo yenew makao yake katika kaunti ya Bungoma ugani Sudi, spika Wetang’ula aliipa timu hiyo shilingi milioni mbili kupitia usimamizi wa klabu. Hela hizo kwa mujibu wa Wetang’ula zinastahili kusaidia timu hiyo kushughulikia ada za usafiri katika mechi za ugenini kwenye ligi ya NSL.
Spika huyo amesema kwamba ni shabiki wa timu hiyo huku akimtaka mwenyekiti wa klabu hiyo Evans Kadenge kuzidisha kasi ya timu hiyo kwa kuimarisha katika mazoezi na utaalamu wa ujuzi.
“Nimemhimiza mwenyekiti Evans Kagenge kuendelea kuweka kasi ya klabu kupitia kuimarisha timu katika mazoezi na utaalamu wa ujuzi.” Alisema Spika Weatang’ula kwenye ukurasa wake wa X.
Wetang’ula ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wengine kutoka kaunti ya Bungoma, aliwataka viongozi kote nchini kuwahimiza vijana kutanua ujuzi wao ikiwemo kwenye michezo ili kufaidi kiuchumi na ki afya.
Kwa upande wa usimamizi wa Nzoia Sugar FC, wameelezea furaha
yao kwa viongozi wa kisiasa kutoka kaunti ya Bungoma kwa kujitokeza kuisadia
timu hiyo.