Kocha wa Harambee Stars Engin Firat amejuizulu wadhfa wake wa kuiongoza timu ya taifa ya kandanda ya wanaume ya Kenya siku chache baada ya Hussein Mohamed na MacDonald Mariga kutangazwa washindi wa urais na unaibu rais wa shirikisho la soka nchini FKF.
Engin Firat ambaye ameongoza Harambee Stars kwa muda wa zaidi ya miaka 3, alibeba kombe la mashindano ya nchi nne iliyofanyika nchini Malawi mwaka huu.
Kabla ya kujuizulu kwake, Firat alikuwa amedokeza kwamba alikuwa na mipango mizuri ya timu ya taifa ikiwa Doris Petra na Nick Mwendwa wangechaguliwa tena kuongoza FKF.
“Nilizungumza na rais Nick Mwendwa, na kama Doris Petra atachaguliwa, tutakaa na kuweka mipango ya mwaka ujao. Tuna malengo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mashindano jijini Nairobi. Lakini tutaona kitakachotokea baada ya uchaguzi,” Alisema Firat baada ya mechi ya mwisho ya kufuzu AFCON dhidi ya Namibia nchini Afrika Kusini.
Kocha huyo amekuwa kwenye shinikizo kutoka kwa washikadau wa soka nchini haswa mashabiki, waliomtaka kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya na kukosa kuiongoza Harambee Stars kufuzu Kombe la mataifa barani Afrika AFCON ya mwaka 2025 itakayofanyika nchini Morocco.
Vile vile, waziri wa michezo Kipchumba Murkomen akiwa mbele ya kamati maalum ya bunge ya kuangazia michezo, awali alikuwa amesema kwamba alifahamu kuwepo kwa makubaliano baina ya shirikisho la soka nchini na Engin Firat kwamba ikiwa Kenya ingalikosa kufuzu AFCON 2025.mkataba wa Engin Firat ungefika kikomo.