Estevao ndiye kinda na chipukizi wa hivi punde mwenye mvuto zaidi katika soka la Brazil, akifuata nyayo za mchezaji mwenzake wa zamani Endrick, ambaye sasa anachezea Real Madrid.
Winga huyo, ambaye alivunja rekodi ya Neymar ya Brasileirao kwa kuhusika kwa mabao mengi zaidi na mchezaji mwenye umri wa miaka 17 au chini zaidi mwezi Oktoba, tayari amekubali kujiunga na Chelsea kwa mkataba utakaoanza kwa pauni milioni 29 na unaweza kupanda hadi pauni milioni 52. Lakini sheria za uhamisho wa kimataifa zinaashiria kuwa kinda huyo hawezi kuhama kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Huku msimu wa 2024 wa Brazil ukikamilika, Estevao anatarajiwa kusafiri hadi London kutembelea klabu ya Chelsea msimu huu wa baridi. Hata akipanga kuizuru klabu hiyo, Estevao alifichua kuwa tayari anafanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ya klabu hiyo.
Alidokeza kwamba miongoni mwa wachezaji wa Chealsea wanaongea na yeye ni pamoja na Cole Palmer na Nahodha wa timu hiyo Reece James Kupitia mtandao wa instagram.
Mchezaji huyo aliongezea kuwa ameambiwa mambo mazuri na sifa nzuri kuhusu klabu hiyo na aliyekuwa mchezaji na Nahodha wa The Blues Thiago Silva ambaye anaichezea Fluminense.
‘’ Niliongea na Thiago Silva katika mchuano wa mwisho. Alisema kuwa klabu iko imara na wanagoja kunikaribisha kwa furaha zaidi,’’ alisema Estevao.
Kinda huyo alisema kuwa anaendelea kujifunza kiingereza kama baadhi ya matayarisho ya kujiunga na timu ya Chelsea.
‘’ Najifunza Kiingereza kwa sasa japo kuwa si rahisi ila ni mbinu nzuri hasa kutazama filamu bila manukuu. Sijatembelea klabu ya Chelsea bado lakini nikipata nafasi ya likizo ntaweza kutembelea klabu hiyo,’’ lisema Estevao.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 17 aliifungia Palmeiras bao la ushindi dakika ya 73 dhidi ya Gremio na kuwa mchezaji wa kwanza wa chini ya miaka 18 katika historia ya Serie A ya Brazil kuandikisha mabao 20 na kuzalisha mabao katika msimu mmoja. Amefunga mabao 12 na kuzalisha mabao nane katika kampeni za 2024-25.