Makocha wawili wanaosimamia timu za Ligi Kuu ya Uingereza walipoteza kazi zao wikendi baada ya kusajili vipigo.
Wolverhampton Wanderers ilimfuta kazi meneja wao Gary O’Neil Jumamosi jioni baada ya kupoteza 1-2 dhidi ya Ipswich Town huku Southampton ikimtimua Russel Martin saa chache baadaye kufuatia kichapo cha 0-5 dhidi ya Tottenham Hotspurs.
Southampton ilithibitisha kumfuta kazi Martin siku ya Jumapili jioni na kutangaza kuwa meneja wa vijana wa chini ya umri wa miaka 21 Simon Rusk ataisimamia timu hiyo kwa muda.
"Tunaweza kuthibitisha kwamba tumechukua uamuzi mgumu kutengana na Meneja wetu wa Timu ya Kwanza ya Wanaume, Russell Martin," Southampton ilitangaza katika taarifa.
"Tungependa
kuchukua fursa hii kumshukuru Russell na wafanyakazi wake kwa kazi ngumu na
kujitolea ambao wameipa klabu ndani na nje ya uwanja katika kipindi cha miezi
18 iliyopita. Kila mtu anayehusishwa na Southampton FC daima atakuwa na
kumbukumbu nzuri za msimu uliopita, hasa ushindi wa Fainali ya Play-Off mwezi
Mei. Meneja wa sasa wa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 21, Simon Rusk
atachukua jukumu la kuinoa timu kwa muda hadi tutakapotangaza mbadala wa
kudumu,” taarifa hiyo ilitangaza zaidi.
Wolves pia ilithibitisha kutimuliwa kwa Gary O’Neil Jumapili asubuhi na kumshukuru kwa michango yake tangu kuteuliwa Agosti mwaka jana.
"Wolves wametengana na kocha mkuu Gary O'Neil na wafanyikazi wake wa nyuma," Wolves walitangaza.
Timu hizo mbili kwa sasa ziko mkiani mwa jedwali Wolves kwa alama 24 na Southampton kwa alama 5.