Kiungo mkavaji wa klabu ya Chelsea Moises Caicedo amekiri kwamba kwenye taaluma yake, N’Golo Kante ndiye mchezaji anayemtazamia sana.
Akizungumza baada ya mchezo wa Chelsea dhidi ya Brentford ugani Stamford Bridge, mchezaji huyo raia wa Ecuador, alisema kwamba wakati wote huwa anajaribu kucheza vizuri jinsi Kante alikuwa anacheza ili kuisaidia Chelsea kuandikisha matokeo bora.
Chelsea ilimnunua mchezaji huyo kutokea timu ya Brighton and Hove Albion mnamo mwaka wa 2021 ili kuziba pengo la mchezaji N’Golo Kante aliyeondoka kuelekea Uarabuni.
Katika msimu huu wa 2024/2025 kufikia Disemba 16, Caicedo amecheza jumla ya mechi 16 na kuifungia Chelsea bao moja sawia na kuchangia mabao mawili katika mashindano yote ambayo Chelsea imeshiriki msimu huu.
Akizungumza na wanahabari baada ya mechi ya raundi ya 16 ya ligi kuu nchini Uingereza, ambapo Chelsea ilishinda kwa mabao mawili dhidi ya moja, Caicedo alimtaja N’Golo Kante kuwa mchezaji mkubwa sana.
“N’Golo Kante ni sanamu yangu. Najaribu kusaidia Chelsea jinsi alikuwa anafanya… ni mchezaji mkubwa sana, najaribu ubora wangu.” Alisema Moises Caicedo.
Aidha mchezaji huyo vile vile alisema kwamba anafurahia mchezo wa Chelsea na timu inafanya vyema katika mechi zake akiashiria kwamba anga ndio kikomo chao.
Chelsea baada ya michuano 16 ya ligi kuu Uingereza,
inashikilia nafasi ya 2 kwa alama 34 alama 2 nyuma na viongozi Liverpool licha
ya wao kuwa wamecheza mechi 15. Chelsea imeweka mwanya wa pointi 4 na nafasi ya
tatu Arsenal ambao wanatoshana kwa alama na Manchester City.