Katika mchuano wa debi kati ya Manchester city na Manchester
United kocha wa timu ya Manchester United Ruben Amorim aliamua kuwaacha nje
ya kikosi hicho Marcus Rashford na Alejandro Garnacho hatua ambayo iliibua maswali
miongoni mwa mashabiki.
Marcus Rashford na Alejandro Garnacho ambao hawakusafiri pamoja na wachezaji wengine wa Man United ugani Etihad kwa ajili ya mechi kubwa ya debi dhidi ya City licha ya kutokuwa na majeraha wala kupata kadi iliwaacha mashabiki wa the Red Devils na maswali mengi.
Mkufunzi huyo alipoulizwa sababu ya kuwaacha nje wachezaji hao wawili ambao kwa kawaida huwa miongoni mwa kikosi cha wachezaji kumi na moja wa kuanza mechi kadhaa za Manchester United, alisema kuwa uamuzi huo aliufanya kulingana na utathmini wa michango ya jumla ya wachezaji ndani na nje ya uwanja.
‘’Tunajaribu kutathmini kila kitu, mazoezi, utendaji kazi, uhusiano na wachezaji wenza, kila kitu kiko poa tunapochambua na kuchagua wachezaji, kwa hivyo ilikuwa chaguo langu. Rahisi hivo,’’ Alisema Amorim akihojiwa na kituo cha habari ya Sky Sports.
Kocha huyo Mreno alieleza kuwa anatathmini mambo mengi bali si utendaji kazi pekee wa mchezaji uwanjani, Aliongeza kuwa anaangalia heshima na utaaluma wa mchezaji pia. Amorim alikinai madai kuwa uamuzi wake wa kuwaacha baadhi ya wachezaji ni njia moja ya kuwaonya wachezaji wengine.
“Ninazingatia kila kitu, jinsi unavyokula, unavyovaa nguo ukienda kwenye zoezi. Kila kitu. Ninafanya tathmini yangu, na kisha lazima niamue. Nina wachezaji wengi wa kuchagua, na leo nimefanya chaguo langu. Sitaki kutuma kujumbe, ni tathmini tu na hata wachezaji wangu wanaijua,’’ Alisema Ruben.
Hata hivyo, Amorim alikiri kuwa ni ngumu kuchukua hatua kama hizo hasa wakati wa kipindi kigumu kwa timu hiyo.
Katika mchuano huo, Manchester United waliwacharaza vijana wa Guardiola mabao mawili kwa moja licha ya Josko Gvardiol kufunga bao la kwanza katika dakika ya 36 na kuiweka City kifua mbele mpaka dakika ya 88 wakati nahodha wa timu hiyo Bruno Fernandes alifunga bao la kwanza kupitia matuta ya penalti.
Katika dakika ya 90, Amad Diallo alifunga bao la pili la ushindi. Winga huyo mdogo alionesha uimairi wake na kuiona Manchester United chini ya Mkufunzi Ruben Amorim wakipata ushindi ugani Etihad baada ya miaka miwili.