Klabu ya soka ya Manchester City inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza imeomboleza kifo cha shabiki wao mmoja mwenye umri wa miaka 70 ambaye inaripotiwa alifariki baada ya kuanguka kwenye stendi wakati wa mechi kali ya Manchester Derby mnamo Jumapili jioni.
City ilipoteza kwa vijana wa Ruben Amorim 1-2 katika mechi hiyo kubwa iliyochezwa katika uwanja wa Etihad, na kuwaacha katika nafasi ngumu katika mbio za ubingwa wa EPL 2024/25.
Klabu hiyo ilithibitisha kifo cha shabiki wake kupitia majukwaa rasmi ya mtandaoni na kuwapa pole familia na marafiki wa marehemu.
"Manchester City wanafahamu habari za kusikitisha kwamba mmoja wa wafuasi wetu aliaga dunia kufuatia tukio la kiafya kwenye mechi ya jana. Mawazo ya kila mtu kwenye Klabu yako pamoja na familia na marafiki zao katika wakati huu mgumu sana,” City ilitangaza kwenye Twitter.
Inaelezwa kuwa marehemu alikuwa na umri wa miaka 70 wakati wa kifo chake na alikuwa akiishabikia Man City maisha yake yote.
Inasemekana alipata mshtuko wa moyo wakati wa mechi na kusababisha kifo chake.
Mabingwa hao wa EPL 2023/24 walipoteza mchuano wa Jumapili kufuatia bao la dakika za lala salama la Man United lililofungwa na Amad Diallo.
City walikuwa wanaongoza 1-0 hadi dakika ya 88 shukrani kwa bao la kichwa la Josko Gvardiol lakini Diallo akashinda penalti - ambayo Bruno Fernandes alifunga na kusawazisha - kabla ya kufunga bao la kumalizia mchezo la Diallo katika dakika za lala salama.
Kikosi cha Pep Guardiola sasa kimepoteza michuano minane kati ya 11 iliyopita katika mashindano yote, na kushinda mchezo mmoja pekee kati ya hizo.