Shirikisho la soka barani Afrika, CAF limetangaza kuwa limeimarisha kiwango cha pesa kinachotolewa kwa mshindi wa mashindano ya mataifa barani CHAN.
CAF katika ujumbe wake imesema kwamba pesa za tuzo kwa mshindi kwenye mashindano ya CHAN zimeongezwa kwa asilimia 75. Ongezeko hilo litatolewa katika Makala ya CHAN yatakayofanyika mwezi Februari katika mataifa ya Afrika Mashariki ya Kenya, Uganda na Tanzania.
Aidha mbali ya kuongezwa kwa tuzo ya mshindi, CAF imesema kwamba kiwango jumla cha tuzo zinazotolewa na shirikisho hilo zimeongezwa kwa asilimia 32.
Kutokana na ongezeko hilo, mshindi wa CHAN katika mashindano ya Februari sasa atapokea kitika cha dola milioni 3.5 sawia na shilingi milioni 451.5 za Kenya au shilingi bilioni 8.645 za Tanzania.
Hata hivyo zaidi ya dola milioni 10.4 zitawania kwenye mashindano hayo.
Kwa mujibu wa rais wa CAF Patrice Motsepe, mashindano ya CHAN ni muhimu katika ukuaji wa wachezaji wa soka barani Afrika inayochangia ushindani wa kimataifa wa soka la Afrika.
“Mashindano haya ni sehemu ya mkakati wetu wa kuwekeza katika soka la Afrika na kuifanya kuvutia na kuvutia mashabiki wa soka, watazamaji wa TV, wadhamini, washirika na wadau wengine barani Afrika na duniani kote.” Alisema Patrice Motsepe.
Jumla ya timu 19 zitawania tuzo hiyo ambayo imeongezwa. Tayari timu kumi na saba zilifuzu kushiriki kipute hicho kitakachokamilika Ijumaa, Februari 28 kwa mechi ya fainali.
Kenya, Tanzania, Uganda, Guinea, Morocco, Niger, Mauritania,
Senegal, Burkina Faso, Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Zambia, Congo, Angola na Madagascar tayari
zilifuzu timu mbili zikisalia kufuzu katika michuano iliyosalia.