logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Jinsi majambazi wenye silaha walivyovamia nyumba ya Aubameyang familia yote ikiwa ndani

Tukio hilo halikuacha tu makovu ya kimwili bali pia majeraha makubwa ya kisaikolojia ndani ya familia yake.

image
na Samuel Mainajournalist

Football09 January 2025 - 08:14

Muhtasari


  • Aubameyang alieleza kwa kina jinsi mtoto wake mkubwa alivyomtahadharisha kuhusu kuwepo kwa wavamizi hao.
  • Shambulio hilo liliiacha familia ya Aubameyang ikiwa na majeraha ya kisaikolojia.


Mshambulizi wa zamani wa Arsenal, Chelsea na Borrusia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang alikumbana na matukio ya kutisha sana alipokuwa akiichezea FC Barcelona miaka miwili iliyopita.

Mnamo Agosti 2022, genge la majambazi waliojihami waliingia ndani ya nyumba yake katika mjio wa Castelldefels, Uhispania, wakati familia yake ikiwa ndani, na kuwaweka katika hali ya kuogofya.

Tukio hilo halikuacha tu makovu ya kimwili bali pia majeraha makubwa ya kisaikolojia ndani ya familia yake.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na The Athletic, mchezaji huyo wa kimataifa wa Gabon alieleza kwa kina jinsi mtoto wake mkubwa alivyomtahadharisha kuhusu kuwepo kwa wavamizi hao.

“Mwanangu alikuja mbio na kuniambia, ‘Baba, kuna wavamizi fulani ndani ya nyumba.’ Waliingia kutoka nje, ambapo mke wangu alikuwa akivuta sigara pamoja na binamu yangu na mpenzi wake. Wakamchukua yule mpenzi wa binamu yangu kisha wakaingia ndani. Mke wangu alikuwa akipiga kelele. Walikuwa na bunduki,” Aubameyang alisimulia.

Wakati wa shambulizi hilo, Aubameyang alijaribu kujilinda kwa kutumia chupa kubwa, lakini majambazi hao walimpiga huku wakitishia familia yake.

Shambulio hilo liliiacha familia ya Aubameyang ikiwa na majeraha ya kisaikolojia.

“Baada ya hapo, watoto wangu wangesema, ‘Baba, sitaki kwenda shuleni, ninaogopa jambo fulani linaweza kutokea.’ Mtoto wangu mdogo hakuweza kulala peke yake kwa mwaka mmoja,” alisema.

Mchezaji huyo alikiri kwamba matukio hayo yaliathiri hata utaratibu wake wa kila siku, na kusababisha kukosa usingizi usiku kutokana na hofu na kumbukumbu za mara kwa mara za mashambulizi.

Licha ya zaidi ya miaka miwili kupita tangu tukio hilo, Aubameyang na familia yake hawajarejea katika nyumba yao ya zamani katika eneo la Barcelona.

"Bado nina nyumba hiyo, lakini sijarudi tangu wakati huo. Nafikiri nitaikodisha kwa sababu watoto wangu hawataki kurudi,” alisema.

Uamuzi huu unaonyesha jinsi wizi huo ulivyoathiri maisha ya familia yake, haswa watoto wake ambao bado wanakataa kuzuru jiji hilo.

Mwanasoka huyo ambaye sasa anachezea Al-Qadisiyah nchini Saudi Arabia, alitafakari jinsi ambavyo angeweza kushughulikia hali hiyo kwa hisia.

“Nilifanya makosa kwa kutotafuta usaidizi wa kitaalamu. Ikiwa ningekuwa na mtaalamu au mwanasaikolojia, labda ningeweza kukabiliana nayo vizuri zaidi. Lakini wakati huo, sikutaka kufanya lolote, nilikuwa nimepotea.”



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved