Kocha wa timu ya taifa la Kenya Francis Kimanzi amekiri kwamba mechi ya Ijumaa kati ya Kenya na visiwa vya Zanzibar itakuwa ngumu ikizingatiwa kuwa Zanzibar watakuwa katika uga wa nyumbani. Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Kenya kucheza ili kufuzu katika hatua inayofuata ikiwa itapata ushindi.
Kufikia sasa Kenya inaongoza msimamo wa jedwali la mashindano hayo kwa alama nne ikifuatiwa na Burkina Faso ambao wana pointi sawia.
Akizungumza katika mahojiano na wanahabari, kocha Kimanzi amekiri kwamba lazima Kenya itilie maanani ubora wake ambao imekuwa nao katika mashindano hayo kufikia sasa.
“Lazima pia tuipatie heshima wapinzani wetu Zanzibar, haswa wanapocheza nyumbani. Mechi itakuwa ngumu zaidi lakini cha muhimu ni tuweke (sisi) maanani ubora wetu kama team Kenya.” Alisema Francis Kimanzi.
Harambee Stars katika mechi mbili za awali, imetoka sare moja dhidi ya Burkina Faso kwa kufungana bao moja kwa moja na kushinda mechi ya pili dhidi ya Tanzania Bara kwa mabao mawili kwa nunge. Mabao ya Harambee Stars dhidi ya Tanzania yaligfungwa na Boniface Muchiri wa Ulinzi Stars na Ryam Ogam wa Tusker FC.
Aidha Kimanzi vile vile amesema kwamba ana Imani ya kupata
ushindi kwenye mechi hiyo dhidi ya Zanzibar kutokana na Imani ya timu hiyo kuwa
kila mechi wanayocheza ni muhimu kwao.
Harambee Stars inashiriki kipute cha kombe la
Mapinduzi kwa matayarisho ya mashindano ya mataifa ya barani Afrika CHAN yatakayoandaliwa nchini kwa ushirikiano na Tanzania na Uganda kuanzia Februari
mosi hadi Februari 28.