logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mkewe Kai Havertz asikitika baada ya mashabiki wa Arsenal kumtakia kifo mtoto aliyebeba tumboni

Baadhi ya Mashabiki walimtumia mkewe Havertz jumbe za vitisho baada ya mshambulizi huyo kukosa penalti.

image
na Samuel Mainajournalist

Football13 January 2025 - 08:12

Muhtasari


  • Mkewe Havertz alielezea kusikitishwa kwake na jumbe za vitisho ambazo mashabiki walimtumia baada ya mumewe kukosa penalti.
  • Bi Sophia alifichua jumbe mbili alizopokea, ambazo zote zilionekana kumtakia mabaya mtoto wake ambaye hajazaliwa.


Sophia Weber, mke wa mshambuliaji wa Arsenal Kai Havertz, mnamo Jumapili jioni alielezea kusikitishwa kwake baada ya baadhi ya wanamtandao kumtumia jumbe za vitisho kufuatia kupoteza kwa Wanabunduki kwa Manchester United kwenye uwanja wa Emirates.

Mashetani Wekundu waliwabandua vijana wa Mikel Arteta nje ya mashindano ya Kombe la FA wakiwa na wachezaji 10 baada ya mlinzi Diogo Dalot kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kadi ya pili ya njano katika kipindi cha pili cha mechi. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya 1-1, ikatoka bila bao katika muda wa nyongeza, huku United wakifunga penalti zao zote na kushinda mechi hiyo.

Kai Havertz, aliyepiga penalti ya pili kwa Arsenal, hakuweza kufunga, huku mlinda mlango wa United, Altay Bayindir akidaka. Huenda kukosa penalti hiyo ndiyo sababu iliyowafanya baadhi ya mashabiki wa Arsenal kughadhabika na kwenda kumshambulia Havertz na familia yake mtandaoni.

Bi Sophia alifichua jumbe mbili za aibu alizopokea kutoka kwa mashabiki, ambazo zote zilionekana kumtakia mabaya mtoto wake ambaye hajazaliwa.

"Natumai mimba yako iharibike," mtumiaji mmoja wa Instagram alimwandikia mke wa Havertz.

Mwingine aliandika, "Nitakuja nyumbani kwako na kumchinja mtoto wako. Sifanyi mzaha, ngoja tu.”

Huku akijibu jumbe za vitisho ambazo alipokea kwenye Instagram, mke wa Kai Havertz alibainisha kuwa zilikuwa zimemwacha bila maneno ya kusema.

Hata hivyo aliwasihi mashabiki kukoma kutuma jumbe hizo na kutenda kwa njia ya heshima zaidi.

"Sina hakika hata niseme nini lakini tafadhali nyie muwe na heshima zaidi. Sisi ni bora kuliko hii..” Sophia aliandika.

Nahodha wa Arsenal Martin Odegaard alifunga penalti ya kwanza ya timu hiyo kabla ya Kai Havertz kupoteza nafasi yake.

Declan Rice na Thomas Partey walifunga nafasi zao lakini haikutosha kuwapa Wanabunduki ushindi kwani United walifunga nafasi zao zote.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved