logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Fahamu timu za CHAN 2025 baada ya droo kufanyika Nairobi

Mashindano hayo ya kipekee, yanayoleta pamoja wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani pekee, likiwa jukwaa muhimu ya kandanda barani Afrika.

image
na OTIENO TONNY

Football16 January 2025 - 12:00

Muhtasari


  • Hassan Wasswa, Mrisho Ngasa na Mac Donald Mariga hatimaye walitoa droo ambapo Kenya, kama wenyeji, waliangukia  Kundi A.
  •  Tanzania inaongoza Kundi B, ambapo itamenyana na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.


Droo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu  iliyofanyika Jumatano, Januari 15, katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Kenyatta maarufu kama (KICC) jijini Nairobi, Kenya, ilifichua mchujo mkali wa mashindano ya Agosti 2025.

Kwa mara ya kwanza tangia nchi ya Rwanda kuandaa michezo za CHAN mnamo mwaka wa 2016, CHAN inarejea katika ukanda wa Afrika Mashariki huku nchi ya Kenya, Uganda na Tanzania zikiungana  kuandaa mashindano  hayo.

Mashindano hayo ya kipekee, yanayoleta pamoja  wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani pekee, ni jukwaa linalosherehekewa kwa vipaji vya kandanda barani Afrika.

Hassan Wasswa, Mrisho Ngasa na Mac Donald Mariga hatimaye walitoa droo ambapo Kenya, kama wenyeji, waliangukia  Kundi A, kundi lenye uzito linaloshirikisha mabingwa wa zamani Morocco ambao ni washindi kwa mara mbili na DR Congo ambao vilevile ni washindi kwa mara mbili wa taji hilo.

Kundi  la A pia inaleta pamoja timu ya Angola na Zambia. Kundi hilo likiwa na mabingwa wa CHAN watatu wa zamani ni ishara tosha kuwa  litaahidi mchezo wa  kusisimua na ushindani mkali.

Morocco iliibuka mshindi wa CHAN mnamo mwaka wa 2018 na 2020  huku DRC Congo ikishinda taji hilo  mwaka wa 2009 na 2016 .

Timu ya Angola imeshiriki CHAN mara nne na kumalizia katika nafasi wa pili mwaka wa 2011 huku Zambia ambao vilevile wameshiriki mara nne walimaliza katika nafasi ya 3 mnamo 2009.

Tanzania inaongoza Kundi B, ambapo itamenyana na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso, na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kama mojawapo ya waandaji, Tanzania italenga kuongoza na kupata matokeo mazuri ikilinganishwa kuwa watakuwa  na faida ya nyumbani na mashabiki wengi.

Katika kundi la B hakuna hata timu moja ambayo imetua taji ya CHAN hii ikiwa ni nafasi murwa wa timu hizo kujaribu kupata ushindi wa kwanza wa mashindano hayo.

Kundi la C linatoa mchanganyiko wa changamoto zinazojulikana na zisizojulikana kwa wenyeji Uganda. The Cranes itakutana na Niger, Guinea, na timu mbili ambazo bado hazijafuzu.

Huku nafasi kadhaa zikiwa zimefunguliwa, mienendo ya mwisho ya kundi hilo itategemea matokeo ya mechi za kufuzu zinazoendelea zinazohusisha Algeria, Comoro, Gambia, Malawi, Misri, Afrika Kusini, na Gabon.

Katika hilo kundi la Uganda timu mbili pekee ndio zimedhibitishwa kukutana na The Cranes ikiwa ni Niger na Guinea. Zote zikiwa bado na matumaini ya kuwa mabingwa wa taji la CHAN.

Mabingwa watetezi Senegal inaongoza kundi la D, huku imeratibiwa kumenyana na Congo, Sudan, na Nigeria. Kama washindi wa hivi majuzi, Senegal inaingia ikiwa na matarajio makubwa, lakini itakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani.

Congo imefuzu kwa mashindano hayo mara mbili na zote ikiiona kuondolewa katika awamu  ya makundi huku Sudan imeshiriki mara tatu, kumaliza katika nafasi ya tatu mara mbili na kuondolewa katika awamu ya makundi mara moja.

Nigeria ambayo vilevile imeshirika katika CHAN mara tatu imepata nafasi ya kumaliza katika nafasi ya pili mnamo mwaka wa 2018, nafasi ya tatu mwaka wa 2014 na kuondolewa katika awamu ya makundi mwaka wa 2016.

Kufikia 2025, timu tano pekee zimetua taji la CHAN ikiwemo DRC Congo mara mbili (2009,2016), Libya (2014), Morocco mara mbili (2018,2020), Senegal (2022) na Tunisia (2011).


 


 


 


 


 


 



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved