Ole Gunnar Solskjaer mwenye umri wa miaka 51 ndiye kocha
mpya wa Besiktas baada ya kutua Instanbul na kusaini kandarasi ya mwaka moja na
nusu na timu hiyo ya Uturuki na sasa amerejea katika ukufunzi baada ya kuachana na United mwaka
wa 2021.
Kwa mujibu wa 'Sports Digitale', mchezaji na bosi huyo wa zamani wa Man United alitua Istanbul kwa ajili ya kuandikisha mkataba wa mwaka mmoja na nusu na Besiktas ambao unamfanya achukue mikoba ya meneja wa muda Serdar Topraktepe.
Solskjaer sasa yuko tayari kukabiliana na Jose Mourinho, ambaye ndiye mkufunzi wa Fenerbahce.
Solskjaer alichukua nafasi ya Mourinho kama kocha kwa muda kule United mnamo Desemba 2018 kabla ya kuchukua jukumu la kuwa Kocha rasmi wa Red Devils mnamo Machi 2019.
Mraia huyo wa Norway akiwa dimbani kwa misimu miwili kamili, Manchester United walishika nafasi ya tatu na ya pili kwenye Ligi ya premia ya Uingereza na kutinga fainali ya Ligi ya Europa mnamo mwaka wa 2021 na baadaye kupoteza dhidi ya Villarreal kwa mikwaju ya penalti.
Timu hiyo ya Uturuki, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 30 kwenye msimamo wa Super Lig, imekuwa bila meneja wa kudumu tangu kuondoka kwa Giovanni van Bronckhorst mwezi Novemba mwaka jana . Mholanzi huyo alidumu kwa miezi mitano pekee kwenye usukani kabla ya kutimuliwa na klabu hiyo.
Raia huyo wa Norway amekuwa hana kazi tangu alipotimuliwa na Man Utd mnamo Novemba 2021, lakini ametambulishwa kama kocha wa kudumu na kuchukua nafasi ilioachwa na Giovanni van Bronckhorst.
Akiongea na ‘ TRT spor’ Ole Gunnar alionyesha furaha yake ya kurejea katika kazi ya ukufunzi na vilevile kuridhishwa na uteuzsi wake kama kocha mpya wa timu ya Besiktas.
‘’Inapendeza kuwa hapa na inapendeza kuona watu wengi wakijali uwepo wa klabu hii nzuri, Kwangu, nimekuwa na mkutano mzuri sana wa kwanza na wadsimamizi wa bodi hapa na ninamatumaini sana. Inafurahisha kuwa katika jiji hili zuri pia,’’ Hii ni ujumbe wa Ole Gunnar akiongea na sauti ya TRT Spor.
Uteuzi wa Solskjaer katika klabu ya Besiktas unakuwa ndiyo kazi yake ya kwanza ya ukocha tangu kuondoka Man United Novemba 2021