Manchester City wanakaribia kumsajili mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt Omar Marmoush.
Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kuwa makubaliano ya awali yamefikiwa kati ya vilabu hivyo lakini uhamisho huo bado haujakamilika.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao 15 katika Ligi ya Bundesliga msimu huu.
Marmoush alijiunga na Eintracht kwa uhamisho wa bila malipo kutoka klabu nyingine ya Bundesliga Wolfsburg mnamo 2023.
Vile vile, Manchester City wanatarajiwa kukamilisha usajili wa beki wa Kibrazil Vitor Reis hivi karibuni, ambaye yuko mbioni kufanyiwa vipimo vya afya ili kukamilisha uhamisho wake kutoka Palmeiras.
Klabu hiyo pia ina nia ya kumsajili beki wa kushoto wa Juventus, Andrea Cambiaso, ingawa vyanzo vya City vinasema kuwa mazungumzo hayajasonga mbele kama ripoti za Italia zinavyopendekeza na hakuna uhakika kwamba uhamisho huo utakamilika mwezi huu.
Cambiaso, 24, alijiunga na Juventus kutoka Genoa mwaka 2022, na msimu huu amecheza mechi 25, akifunga mara mbili na kutoa usaidizi wa kufunga mabao mara mbili.
Mabingwa hao wa Ligi ya Primia bado hawajathibitisha kuwa wamemsajili beki wa Uzbekistan Abdukodir Khusanov, baada ya kuafikiana na Lens kwa ada ya £33.6m kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20.