Staa
wa zamani wa Tottenham na Everton, Dele Alli amesajiliwa na klabu ya Como ya
Italia kwa mkataba wa miezi 18, kukiwa na chaguo la kuongeza muda kulingana na uchezaji
wake.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa akifanya mazoezi na klabu hiyo ya Serie A inayoongozwa na kocha Cesc Fabregas kwa mwezi uliopita kabla ya kukamilisha dili siku ya Jumapili, Januari 19.
"Klabu inaamini uwezo wa Dele na imejitolea kumsaidia kugundua upya kiwango chake bora," alisema kocha mkuu wa Como Cesc Fabregas kufuatia kukamilika kwa mkataba huo.
Alli amekuwa hana klabu tangu alipoondoka rasmi Everton mwezi Juni lakini aliendelea na mazoezi chini ya Sean Dyche kabla ya kujiunga na Como kwa majaribio.
Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uingereza hajashiriki katika mechi ya mashindano tangu Februari 2023, alipokuwa kwa mkopo katika klabu ya Besiktas ya Uturuki.
"Uzoefu wake na sifa za uongozi bila shaka zitanufaisha kikosi. Lengo litakuwa kumpa Dele mazingira ya usaidizi ambapo anaweza kujumuishwa kikosini hatua kwa hatua,” Como ilisema katika taarifa yake.
"Ingawa hakutakuwa na matarajio ya uchezaji bora wa haraka, klabu ina imani kwamba atatoa mchango mkubwa uwanjani na kama mshauri kwa vipaji vya vijana wa klabu," taarifa hiyo ilisema zaidi.
Alli alithibitisha kuondoka kwake Everton mwezi uliopita, katika taarifa ya hisia mtandaoni.
Alisema: "Imekuwa safari ngumu sana kujaribu kuweka vipande vya mwisho pamoja ili kurejesha utimamu wa mechi na siwezi kuwashukuru wafanyakazi wa Everton vya kutosha kwa kazi kubwa waliyoweka katika mchakato huo. Kwa bahati mbaya, mambo hayajafanyika kama sisi sote tulivyotarajia na nadhani ni wakati mwafaka kwangu kufungua ukurasa mpya. Nataka kuwatakia kila la heri katika klabu hii ya ajabu na ninatumai tutaonana tena hivi karibuni."
Como kwa sasa wako katika nafasi ya 17 kwenye jedwali la Serie A wakiwa na pointi 19. Watamenyana na Udinese siku ya Jumatatu.