Nahodha
wa Manchester City Kyle Walker amekamilisha uhamisho wa kujiunga na klabu ya AC
Milan ya Italia kwa mkopo kwa muda uliosalia wa msimu wa 2024/25.
Beki huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 34 alikamilisha vipimo vya afya na wababe hao wa Serie A siku ya Alhamisi kabla ya kutambulishwa rasmi.
Dili la Milan kwa Walker linajumuisha chaguo la kumnunua mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs wakati mkataba wake wa mkopo utakapokamilika mwishoni mwa msimu.
Walker ambaye ni mshindi mara sita wa Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na City, anaungana na Waingereza wenzake Fikayo Tomori, Ruben Loftus-Cheek na Tammy Abraham kwenye uga wa San Siro.
Atavaa jezi nambari 32 huko Milan, na anaweza kucheza mechi yake ya kwanza watakapoikaribisha Parma katika Serie A Jumapili.
Kufuatia uhamisho wake, Walker aliandika barua ndefu na yenye hisia kali kwa wenzake katika City, mashabiki na makocha wa klabu hiyo baada ya kuthibitishwa kuondoka kwake akisema kwamba kusajiliwa kwa klabu hiyo imekuwa ndoto.
"Shukrani kubwa kwa watu wengi, wakufunzi, wahudumu wa vifaa na wafanyikazi wote wa nyuma ambao wanafanya kazi bila kuchoka nyuma ya pazia. Mnafanya kila siku kufurahisha na kutoa jukwaa kwa sisi kufanya bora," Walker aliandika kwenye Instagram.
"Kwa wachezaji wenzangu, tangu nilipopitia mlangoni nilihisi niko nyumbani. Asanteni kwa kumbukumbu nzuri na mafanikio tuliyoshiriki pamoja. Nyinyi ni marafiki, lakini pia familia ya maisha. Kwa Pep Guardiola, asante kwa kuniamini na kufanya kazi kwa bidii kunileta hapa mwaka wa 2017. Pamoja, tumesherehekea makombe 17, na mwongozo wako umenisaidia kuwa mchezaji niliye leo nashukuru,” aliongeza.
Walker
ameichezea City mechi 319 tangu uhamisho wa £50m kutoka Tottenham mwaka 2017 na
alikuwa sehemu ya timu iliyoshinda mara tatu msimu wa 2022-23.
Beki huyo wa kulia, ambaye ameichezea Uingereza mechi 93, amekuwa sehemu ya vikosi vyote sita vilivyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza chini ya Pep Guardiola kwenye Uwanja wa Etihad.
Walker alicheza mara ya mwisho tarehe 4 Januari dhidi ya West Ham lakini alimfahamisha meneja Guardiola baada ya mchezo kuwa anataka kuondoka klabuni hapo.