Kiungo wa kati wa Harambee Stars Timothy Ouma hatimaye ametambulishwa kama mchezaji mpya wa klabu ya Slavia Prague ya Czech baada ya kukamilisha uhamisho wake wa pesa nyingi kutoka klabu ya Sweden ya Elfsborg.
Ouma alisajiliwa kwa Kronor milioni 40 (Ksh473 milioni) na ameweka kalamu kwenye karatasi kuashiria mkataba wa miaka minne ambao unamalizika Juni 2029, Sasa ataanza ukurasa mpya katika kazi yake.
"Timothy ni mchezaji mdogo, mwenye vipaji, anayewakilisha nchi yake. Tunaamini kwamba atakuwa kiungo muhimu miongoni mwa wachezaji wetu. Ana sifa kubwa za kimwili, anaweza kuharakisha mchezo, ni mzoefu katika kushindania mpira binafsi, "alisema Mkurugenzi wa Michezo wa Slavia Prague Jiri Bilek.
Mabingwa hao wa mara 21 wa Ligi Kuu ya Czech walitangaza kumsajili Timothy Ouma mwenye umri wa miaka 20 katika mitandao yao ya kijamii siku ya Jumapili.
Ouma akiwa kwenye mahojian0 na wanahabari wa timu hio aliserma kwamba
..."Ni hisia kubwa. Ninatarajia kufurahia kwenye uwanja. Kujaribu kuwa mchezaji halali, mchezaji wa kuleta utofauti. Nitajitahidi kwa kila hatua, niaminini.
Uwanja ni mzuri, mkubwa. Nimekuwa tu katika mji huu kwa muda mfupi lakini nimeona kwamba Prague ni nzuri. Hii ni mara yangu ya kwanza kuwa hapa. Nadhani nitakuwa vizuri hapa," alisema Ouma.
"Haikuwa uamuzi rahisi, lakini nilikaa chini na wakala wangu, na mwishowe tulikubaliana kwamba niende hapa. Hivyo Slavia itakuwa chaguo bora kwangu. Slavia ni timu kubwa yenye wawakilishi wengi. Siwezi kusubiri kujiunga na wachezaji. Tutaona jinsi msimu uliobaki utakavyokuwa kwetu sote." alieleza Ouma.
Fununu zinaarifu kwamba kulikuwa na vilabu vingi vya Uingereza na Ufaransa ambavyo vilikuwa vinahitaji huduma zake ila maamuzi aliyoyafanya ndio yalimufurahisha.
Kiungo huyo alijiunga na timu ya Elfsborg mwaka 2022 akitokea klabu ya Nairobi City Stars ya hapa nchini Kenya.
Timothy Ouma alijiunga na Nairobi City Stars mwaka 2020 baada ya kukamilisha masomo yake katika shule ya Laiser Hill Academy.
Aliitwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya taifa Harambee Stars mwaka 2021 wakati Engin Firat alipokuwa mkufunzi wa taifa.