logo

NOW ON AIR

Listen in Live

William Saliba Ajitolea Kucheza Kama Mshambuliaji Baada ya Arsenal Kukumbwa Tatizo La Majeraha

Arsenal sasa inategemea washambuliaji watatu pekee: Leandro Trossard, Raheem Sterling, na chipukizi Ethan Nwaneri.

image
na Samuel Mainajournalist

Football15 February 2025 - 11:34

Muhtasari


  • Arteta, amefichua kuwa beki William Saliba, alijitolea kucheza kama mshambuliaji kufuatia tatizo la majeruhi.
  • Arteta amekiri kuwa beki huyo ana roho ya kupambana na alijitokeza mara moja kujitolea kusaidia mbele.

Beki William Saliba

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amefichua kuwa beki wake tegemeo, William Saliba, alijitolea kucheza kama mshambuliaji kufuatia tatizo la majeruhi lililokumba timu hiyo.

 Arsenal inajiandaa kuvaana na Leicester City siku ya Jumamosi, ikilenga kupunguza pengo la alama kati yao na vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza, Liverpool, hadi pointi nne.

 Hata hivyo, kikosi cha Arteta kimepata pigo kubwa baada ya mshambuliaji wake, Kai Havertz, kupata jeraha na kutangazwa hatashirikishwa kwenye kikosi msimu mzima uliosalia kutokana na jeraha la msuli wa paja.

 Havertz anajiunga na orodha ndefu ya majeruhi ambayo tayari inajumuisha Gabriel Jesus, Bukayo Saka, na Gabriel Martinelli.

 Hii inamaanisha kuwa Arsenal sasa inategemea washambuliaji watatu pekee: Leandro Trossard, Raheem Sterling, na chipukizi Ethan Nwaneri.

Kwa hali hii, Arteta atalazimika kuwa mbunifu katika kupanga safu yake ya ushambuliaji.

 Ingawa ni vigumu kufikiria kocha huyo akimchezesha Saliba kama mshambuliaji wa kweli, Arteta amekiri kuwa beki huyo ana roho ya kupambana na alijitokeza mara moja kujitolea kusaidia mbele.

"Willy ni mtu wa kuchekesha sana," alisema Arteta. "Mara moja alijitokeza na kusema, ‘Nitacheza kama mshambuliaji.’”

Kocha huyo pia alifichua kuwa Saliba aliwahi kucheza kama mshambuliaji alipokuwa mdogo na alikuwa mfungaji mzuri kabla ya kuhamia safu ya ulinzi.

"Ni kweli, alicheza kama mshambuliaji na alikuwa akifunga mabao mengi," aliongeza Arteta.

 Saliba mwenyewe amewahi kueleza kuwa alipoanza soka katika klabu yake ya utotoni, AS Bondy, na baadaye Montfermeil nchini Ufaransa, alikuwa mshambuliaji matata.

 Arteta pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu mzigo mkubwa wa mechi kwa wachezaji wa kisasa, akisema kuwa majeraha ya muda mrefu kama lile la Havertz ni "ajali iliyokuwa ikisubiri kutokea."

 "Tulikuwa na kambi nzuri sana ya mazoezi Dubai, lakini kisha jeraha likatokea kwa njia isiyotarajiwa. Ni pigo kubwa sana kwa sababu ya majeraha tuliyonayo," alisema Arteta.

 Huku mbio za ubingwa zikiendelea kushika kasi, Arsenal italazimika kutafuta mbinu mbadala za kusonga mbele, huku mashabiki wakisubiri kuona iwapo Arteta atamjaribu Saliba kama mshambuliaji wa dharura au la.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved